| ← Psalms (90/150) → |
| 1. | Wewe, Bwana, umekuwa makao yetu, Kizazi baada ya kizazi. |
| 2. | Kabla haijazaliwa milima, wala hujaiumba dunia, Na tangu milele hata milele ndiwe Mungu. |
| 3. | Wamrudisha mtu mavumbini, usemapo, Rudini, enyi wanadamu. |
| 4. | Maana miaka elfu machoni pako Ni kama siku ya jana ikiisha kupita, Na kama kesha la usiku. |
| 5. | Wawagharikisha, huwa kama usingizi, Asubuhi huwa kama majani yameayo. |
| 6. | Asubuhi yachipuka na kumea, Jioni yakatika na kukauka. |
| 7. | Maana tumetoweshwa kwa hasira yako, Na kwa ghadhabu yako tumefadhaishwa. |
| 8. | Umeyaweka maovu yetu mbele zako, Siri zetu katika mwanga wa uso wako. |
| 9. | Maana siku zetu zote zimepita katika hasira yako, Tumetowesha miaka yetu kama kite. |
| 10. | Siku za miaka yetu ni miaka sabini, Na ikiwa tuna nguvu miaka themanini; Na kiburi chake ni taabu na ubatili, Maana chapita upesi tukatokomea mara. |
| 11. | Ni nani aujuaye uweza wa hasira yako? Na ghadhabu yako kama ipasavyo kicho chako? |
| 12. | Basi, utujulishe kuzihesabu siku zetu, Tujipatie moyo wa hekima. |
| 13. | Ee Bwana urudi, hata lini? Uwahurumie watumishi wako. |
| 14. | Utushibishe asubuhi kwa fadhili zako, Nasi tutashangilia na kufurahi siku zetu zote. |
| 15. | Utufurahishe kwa kadiri ya siku ulizotutesa, Kama miaka ile tuliyoona mabaya. |
| 16. | Matendo yako na yaonekane kwa watumishi wako, Na adhama yako kwa watoto wao. |
| 17. | Na uzuri wa Bwana, Mungu wetu, uwe juu yetu, Na kazi ya mikono yetu utufanyie thabiti, Naam, kazi ya mikono yetu uithibitishe. |
| ← Psalms (90/150) → |