← Psalms (89/150) → |
1. | Fadhili za Bwana nitaziimba milele; Kwa kinywa changu nitavijulisha vizazi vyote uaminifu wako. |
2. | Maana nimesema, Fadhili zitajengwa milele; Katika mbingu utauthibitisha uaminifu wako. |
3. | Nimefanya agano na mteule wangu, Nimemuapia Daudi, mtumishi wangu. |
4. | Wazao wako nitawafanya imara milele, Nitakijenga kiti chako cha enzi hata milele. |
5. | Ee Bwana, mbingu zitayasifu maajabu yako, Uaminifu wako katika kusanyiko la watakatifu. |
6. | Maana ni nani katika mbingu awezaye kulinganishwa na Bwana? Ni nani afananaye na Bwana miongoni mwa malaika? |
7. | Mungu huogopwa sana barazani pa watakatifu, Ni wa kuhofiwa kuliko wote wanaomzunguka. |
8. | Bwana, Mungu wa majeshi, Ni nani aliye hodari kama Wewe, Ee YAHU? Na uaminifu wako unakuzunguka. |
9. | Wewe ndiwe ukitawalaye kiburi cha bahari. Mawimbi yake yainukapo wayatuliza Wewe. |
10. | Ndiwe uliyemseta Rahabu akawa kama aliyeuawa, Kwa mkono hodari umewatawanya wakuchukiao. |
11. | Mbingu ni mali yako, nchi nayo ni mali yako, Ulimwengu na vyote viujazavyo Ndiwe uliyeupiga msingi wake. |
12. | Kaskazini na kusini ndiwe uliyeziumba, Tabori na Hermoni hulifurahia jina lako. |
13. | Mkono wako ni mkono wenye uweza, Mkono wako una nguvu, Mkono wako wa kuume umetukuka. |
14. | Haki na hukumu ndio msingi wa kiti chako, Fadhili na kweli zahudhuria mbele za uso wako. |
15. | Heri watu wale waijuao sauti ya shangwe, Ee Bwana, huenenda katika nuru ya uso wako. |
16. | Kwa jina lako hufurahi mchana kutwa, Na kwa haki yako hutukuzwa. |
17. | Maana fahari ya nguvu zao ni Wewe, Na kwa radhi yako pembe yetu itatukuka. |
18. | Maana ngao yetu ina Bwana, Na mfalme wetu ni wake Mtakatifu wa Israeli. |
19. | Ndipo ulipowaambia watakatifu wako kwa njozi, Ukasema, nimempa aliye hodari msaada; Nimemtukuza aliyechaguliwa miongoni mwa watu. |
20. | Nimemwona Daudi, mtumishi wangu, Nimempaka mafuta yangu matakatifu. |
21. | Ambaye mkono wangu utakuwa thabiti kwake, Na mkono wangu utamtia nguvu. |
22. | Adui hatamwonea, Wala mwana wa uovu hatamtesa. |
23. | Bali nitawaponda watesi wake mbele yake, Nitawapiga wanaomchukia. |
24. | Uaminifu wangu na fadhili zangu atakuwa nazo, Na kwa jina langu pembe yake itatukuka. |
25. | Nitaweka mkono wake juu ya bahari, Na mkono wake wa kuume juu ya mito. |
26. | Yeye ataniita, Wewe baba yangu, Mungu wangu na mwamba wa wokovu wangu. |
27. | Nami nitamjalia kuwa mzaliwa wangu wa kwanza, Kuwa juu sana kuliko wafalme wa dunia. |
28. | Hata milele nitamwekea fadhili zangu, Na agano langu litafanyika amini kwake. |
29. | Wazao wake nao nitawadumisha milele, Na kiti chake cha enzi kama siku za mbingu. |
30. | Wanawe wakiiacha sheria yangu, Wasiende katika hukumu zangu, |
31. | Wakizihalifu amri zangu, Wasiyashike maagizo yangu, |
32. | Basi, nitawarudi makosa yao kwa fimbo, Na uovu wao kwa mapigo. |
33. | Lakini fadhili zangu sitamwondolea yeye, Wala sitafanya uaminifu wangu kuwa uongo. |
34. | Mimi sitalihalifu agano langu, Sitalibadili neno lililotoka midomoni mwangu. |
35. | Neno moja nimeliapa kwa utakatifu wangu, Hakika sitamwambia Daudi uongo, |
36. | Wazao wake watadumu milele, Na kiti chake kitakuwa kama jua mbele zangu. |
37. | Kitathibitika milele kama mwezi; Shahidi aliye mbinguni mwaminifu. |
38. | Walakini Wewe umemtupa na kumkataa, Umemghadhibikia masihi |
39. | Umechukizwa na agano la mtumishi wako, Umeinajisi taji yake na kuitupa chini. |
40. | Umeyabomoa maboma yake yote, Umezifanya ngome zake kuwa magofu. |
41. | Wote wapitao njiani wanateka mali zake; Amekuwa laumu kwa jirani zake; |
42. | Umeutukuza mkono wa kuume wa watesi wake; Umewafurahisha wote wanaomchukia. |
43. | Pia umeurudisha nyuma ukali wa upanga wake; Wala hukumsimamisha vitani. |
44. | Umeikomesha fahari yake; Kiti chake cha enzi umekitupa chini. |
45. | Umezipunguza siku za ujana wake; Umemvika aibu. |
46. | Ee Bwana, hata lini? Utajificha hata milele? Ghadhabu yako itawaka kama moto? |
47. | Ukumbuke jinsi mimi nisivyo wa kudumu; Kwa ubatili gani umeiumba jamii ya wanadamu! |
48. | Ni mwanamume gani atakayeishi asione mauti, Atakayejiokoa nafsi yake na mkono wa kuzimu? |
49. | Bwana, zi wapi fadhili zako za kwanza, Ulizomwapia Daudi kwa uaminifu wako? |
50. | Ee Bwana, ukumbuke, Wanavyosimangwa watumishi wako; Jinsi ninavyostahimili kifuani mwangu Masimango ya watu wengi. |
51. | Ambayo adui zako wamesimanga, Ee Bwana, Naam, wamezisimanga hatua za masihi |
52. | Na ahimidiwe Bwana milele. Amina na Amina. |
← Psalms (89/150) → |