Psalms (88/150)  

1. Ee Bwana, Mungu wa wokovu wangu Mchana na usiku nimelia mbele zako.
2. Maombi yangu yafike mbele zako, Uutegee ukelele wangu sikio lako.
3. Maana nafsi yangu imeshiba taabu, Na uhai wangu umekaribia kuzimu.
4. Nimehesabiwa pamoja nao washukao shimoni; Nimekuwa kama mtu asiye na msaada.
5. Miongoni mwao waliokufa nimetupwa, Kama waliouawa walalao makaburini. Hao ambao Wewe huwakumbuki tena, Wametengwa mbali na mkono wako.
6. Mimi umenilaza katika shimo la chini, Katika mahali penye giza vilindini.
7. Ghadhabu yako imenilemea, Umenitesa kwa mawimbi yako yote.
8. Wanijuao umewatenga nami; Umenifanya kuwa chukizo kwao; Nimefungwa wala siwezi kutoka.
9. Jicho langu limefifia kwa ajili ya mateso Bwana, nimekuita kila siku; Nimekunyoshea Wewe mikono yangu.
10. Wafu je! Utawafanyia miujiza? Au waliofariki watasimama na kukuhimidi?
11. Fadhili zako zitasimuliwa kaburini? Au uaminifu wako katika uharibifu?
12. Miujiza yako itajulikana gizani? Au haki yako katika nchi ya usahaulifu?
13. Lakini mimi nimekulilia Wewe, Bwana, Na asubuhi maombi yangu yatakuwasilia.
14. Bwana, kwa nini kuitupa nafsi yangu, Na kunificha uso wako?
15. Nateswa mimi hali ya kufa tangu ujana, Nimevumilia vitisho vyako na kufadhaika.
16. Hasira zako kali zimepita juu yangu, Maogofyo yako yameniangamiza.
17. Yamenizunguka kama maji mchana kutwa, Yamenisonga yote pamoja.
18. Mpenzi na rafiki umewatenga nami, Nao wanijuao wamo gizani.

  Psalms (88/150)