Psalms (86/150)  

1. Ee Bwana, utege sikio lako unijibu, Maana mimi ni maskini na mhitaji
2. Unihifadhi nafsi yangu, Maana mimi ni mcha Mungu. Wewe uliye Mungu wangu, Umwokoe mtumishi wako anayekutumaini.
3. Wewe, Bwana, unifadhili, Maana nakulilia Wewe mchana kutwa.
4. Uifurahishe nafsi ya mtumishi wako, Maana nafsi yangu nakuinulia Wewe, Bwana.
5. Kwa maana Wewe, Bwana, U mwema, Umekuwa tayari kusamehe, Na mwingi wa fadhili, Kwa watu wote wakuitao.
6. Ee Bwana, uyasikie maombi yangu; Uisikilize sauti ya dua zangu.
7. Siku ya mateso yangu nitakuita, Kwa maana utaniitikia.
8. Katikati ya miungu hakuna kama Wewe, Bwana, Wala matendo mfano wa matendo yako.
9. Mataifa yote uliowafanya watakuja; Watakusujudia Wewe, Bwana, Watalitukuza jina lako;
10. Kwa kuwa ndiwe uliye mkuu, Wewe ndiwe mfanya miujiza, Ndiwe Mungu peke yako.
11. Ee Bwana, unifundishe njia yako; Nitakwenda katika kweli yako; Moyo wangu na ufurahi kulicha jina lako;
12. Nitakusifu Wewe, Bwana, Mungu wangu, Kwa moyo wangu wote, Nitalitukuza jina lako milele.
13. Maana fadhili zako kwangu ni nyingi sana; Umeiopoa nafsi yangu na kuzimu.
14. Ee Mungu, wenye kiburi wamenishambulia; Mkutano wa wakatili wamenitafuta roho. Wala hawakukuweka Wewe Mbele ya macho yao.
15. Lakini Wewe, Bwana, U Mungu wa rehema na neema, Mvumilivu, mwingi wa fadhili na kweli.
16. Unielekee na kunifadhili mimi; Mpe mtumishi wako nguvu zako, Umwokoe mwana wa mjakazi wako.
17. Unifanyie ishara ya wema, Wanichukiao waione na kuaibishwa. Kwa kuwa Wewe, Bwana, Umenisaidia na kunifariji.

  Psalms (86/150)