| ← Psalms (85/150) → |
| 1. | Bwana, umeiridhia nchi yako, Umewarejeza mateka wa Yakobo. |
| 2. | Umeusamehe uovu wa watu wako, Umezisitiri hatia zao zote. |
| 3. | Umeiondoa ghadhabu yako yote, Umerudi na kuuacha ukali wa hasira yako. |
| 4. | Mungu wa wokovu wetu, uturudishe, Uikomeshe hasira uliyo nayo juu yetu. |
| 5. | Je! Utatufanyia hasira hata milele? Utadumisha ghadhabu kizazi hata kizazi? |
| 6. | Je! Hutaki kurudi na kutuhuisha, Watu wako wakufurahie? |
| 7. | Ee Bwana, utuonyeshe rehema zako, Utupe wokovu wako. |
| 8. | Na nisikie atakavyosema Mungu Bwana, Maana atawaambia watu wake amani, Naam, na watauwa wake pia, Bali wasiurudie upumbavu tena. |
| 9. | Hakika wokovu wake u karibu na wamchao, Utukufu ukae katika nchi yetu. |
| 10. | Fadhili na kweli zimekutana, Haki na amani zimehusiana. |
| 11. | Kweli imechipuka katika nchi, Haki imechungulia kutoka mbinguni. |
| 12. | Naam, Bwana atatoa kilicho chema, Na nchi yetu itatoa mazao yake. |
| 13. | Haki itakwenda mbele zake, Nayo itazifanya hatua zake kuwa njia. |
| ← Psalms (85/150) → |