| ← Psalms (80/150) → |
| 1. | Wewe uchungaye Israeli, usikie, Wewe umwongozaye Yusufu kama kundi; Wewe uketiye juu ya makerubi, utoe nuru. |
| 2. | Mbele ya Efraimu, na Benyamini, na Manase, Uziamshe nguvu zako, Uje, utuokoe. |
| 3. | Ee Mungu, uturudishe, Uangazishe uso wako nasi tutaokoka. |
| 4. | Ee Bwana, Mungu wa majeshi, hata lini Utayaghadhibikia maombi ya watu wako? |
| 5. | Umewalisha mkate wa machozi, Umewanywesha machozi kwa kipimo kikuu. |
| 6. | Unatufanya sababu ya ugomvi kwa jirani zetu, Na adui zetu wanacheka wao kwa wao. |
| 7. | Ee Mungu wa majeshi, uturudishe, Uangazishe uso wako nasi tutaokoka. |
| 8. | Ulileta mzabibu kutoka Misri, Ukawafukuza mataifa ukaupanda. |
| 9. | Ulitengeneza nafasi mbele yake, Nao ukatia mizizi sana ukaijaza nchi. |
| 10. | Milima ilifunikwa kwa uvuli wake, Matawi yake ni kama mierezi ya Mungu. |
| 11. | Nao uliyaeneza matawi yake hata baharini, Na vichipukizi vyake hata kunako Mto. |
| 12. | Kwa nini umezibomoa kuta zake, Wakauchuma wote wapitao njiani? |
| 13. | Nguruwe wa msituni wanauharibu, Na hayawani wa kondeni wanautafuna. |
| 14. | Ee Mungu wa majeshi, tunakusihi, urudi, Utazame toka juu uone, uujilie mzabibu huu. |
| 15. | Na mche ule ulioupanda Kwa mkono wako wa kuume; Na tawi lile ulilolifanya Kuwa imara kwa nafsi yako. |
| 16. | Umechomwa moto; umekatwa; Kwa lawama ya uso wako wanapotea. |
| 17. | Mkono wako na uwe juu yake Mtu wa mkono wako wa kuume; Juu ya mwanadamu uliyemfanya Kuwa imara kwa nafsi yako; |
| 18. | Basi hatutakuacha kwa kurudi nyuma; Utuhuishe nasi tutaliitia jina lako. |
| 19. | Ee Bwana, Mungu wa majeshi, uturudishe, Uangazishe uso wako nasi tutaokoka. |
| ← Psalms (80/150) → |