| ← Psalms (79/150) → |
| 1. | Ee Mungu, mataifa wameingia katika urithi wako, Wamelinajisi hekalu lako takatifu. Wamefanya Yerusalemu chungu chungu. |
| 2. | Wameziacha maiti za watumishi wako Ziwe chakula cha ndege wa angani. Na miili ya watauwa wako Iwe chakula cha wanyama wa nchi. |
| 3. | Wamemwaga damu yao kama maji Pande zote za Yerusalemu, Wala hapakuwa na mzishi. |
| 4. | Tumekuwa lawama kwa jirani zetu, Mzaha na dhihaka kwao wanaotuzunguka. |
| 5. | Ee Bwana, hata lini? Utaona hasira milele? Wivu wako utawaka kama moto? |
| 6. | Ukali wako uwamwagie mataifa wasiokujua, Na falme za hao wasioliitia jina lako. |
| 7. | Kwa maana wamemla Yakobo, Na matuo yake wameyaharibu. |
| 8. | Usikumbuke juu yetu maovu ya baba zetu, Rehema zako zije kutulaki hima, Kwa maana tumedhilika sana. |
| 9. | Ee Mungu wa wokovu wetu, utusaidie, Kwa ajili ya utukufu wa jina lako. Utuokoe, utughofiri dhambi zetu, Kwa ajili ya jina lako. |
| 10. | Kwa nini mataifa kusema, Yuko wapi Mungu wao? Kisasi cha damu ya watumishi wako iliyomwagika Kijulike kati ya mataifa machoni petu. |
| 11. | Kuugua kwake aliyefungwa Na kuingie mbele zako. Kwa kadiri ya uweza wa mkono wako Uwahifadhi wana wa mauti. |
| 12. | Uwalipe jirani zetu mara saba vifuani mwao Laumu zao walizokulaumu, Ee Bwana. |
| 13. | Na sisi tulio watu wako, Na kondoo za malisho yako, Tutakushukuru milele; Tutazisimulia sifa zako kizazi kwa kizazi. |
| ← Psalms (79/150) → |