← Psalms (78/150) → |
1. | Enyi watu wangu, sikilizeni sheria yangu, Tegeni masikio kwa maneno ya kinywa changu. |
2. | Na nifunue kinywa changu kwa mithali, Niyatamke mafumbo ya kale. |
3. | Mambo tuliyoyasikia na kuyafahamu, Ambayo baba zetu walituambia. |
4. | Hayo hatutawaficha wana wao, Huku tukiwaambia kizazi kingine, Sifa za Bwana, na nguvu zake, Na mambo yake ya ajabu aliyoyafanya. |
5. | Maana alikaza ushuhuda katika Yakobo, Na sheria aliiweka katika Israeli. Aliyowaamuru baba zetu Wawajulishe wana wao, |
6. | Ili kizazi kingine wawe na habari, Ndio hao wana watakaozaliwa. Wasimame na kuwaambia wana wao |
7. | Wamwekee Mungu tumaini lao. Wala wasiyasahau matendo ya Mungu, Bali wazishike amri zake. |
8. | Naam, wasiwe kama baba zao, Kizazi cha ukaidi na uasi. Kizazi kisichojitengeneza moyo, Wala roho yake haikuwa amini kwa Mungu. |
9. | Wale Waefraimu, wenye silaha, wapiga upinde, Walirudi nyuma siku ya vita. |
10. | Hawakulishika agano la Mungu; Wakakataa kuenenda katika sheria yake; |
11. | Wakayasahau matendo yake, Na mambo yake ya ajabu aliyowaonyesha. |
12. | Mbele ya baba zao alifanya mambo ya ajabu, Katika nchi ya Misri, konde la Soani. |
13. | Aliipasua bahari akawavusha; Aliyasimamisha maji mfano wa chungu. |
14. | Akawaongoza kwa wingu mchana, Na usiku kucha kwa nuru ya moto. |
15. | Akapasua miamba jangwani; Akawanywesha maji mengi kama maji ya vilindi. |
16. | Akatokeza na vijito gengeni, Akatelemsha maji kama mito. |
17. | Lakini wakazidi kumtenda dhambi, Walipomwasi Aliye juu katika nchi ya kiu. |
18. | Wakamjaribu Mungu mioyoni mwao Kwa kutaka chakula kwa tamaa zao. |
19. | Naam, walimwamba Mungu, wakasema, Je! Mungu aweza kuandika meza jangwani? |
20. | Tazama, aliupiga mwamba; Maji yakabubujika, ikafurika mito. Pia aweza kutupa chakula? Atawaandalia watu wake nyama? |
21. | Hivyo Bwana aliposikia akaghadhibika; Moto ukawashwa juu ya Yakobo, Hasira nayo ikapanda juu ya Israeli. |
22. | Kwa kuwa hawakumwamini Mungu, Wala hawakuutumainia wokovu wake. |
23. | Lakini aliyaamuru mawingu juu; Akaifungua milango ya mbinguni; |
24. | Akawanyeshea mana ili wale; Akawapa nafaka ya mbinguni. |
25. | Mwanadamu akala chakula cha mashujaa; Aliwapelekea chakula cha kuwashibisha. |
26. | Aliuelekeza upepo wa mashariki mbinguni; Akaiongoza kusi kwa uweza wake. |
27. | Akawanyeshea nyama kama mavumbi, Na ndege wenye mbawa, Kama mchanga wa bahari. |
28. | Akawaangusha kati ya matuo yao, Pande zote za maskani zao. |
29. | Wakala wakashiba sana; Maana aliwaletea walivyovitamani; |
30. | Hawakuachana na matakwa yao. Ila chakula chao kikali ki vinywani mwao |
31. | Hasira ya Mungu ikapanda juu yao, Akawaua waliokuwa wanono; Akawaangusha chini vijana wa Israeli. |
32. | Pamoja na hayo wakazidi kutenda dhambi, Wala hawakuyaamini matendo yake ya ajabu. |
33. | Kwa hiyo akazikomesha siku zao kama pumzi, Na miaka yao kwa hofu ya kuwasitusha. |
34. | Alipowaua ndipo walipokuwa wakimtafuta; Wakarudi wakamtaka Mungu kwa bidii. |
35. | Wakakumbuka kuwa Mungu ni mwamba wao, Na Mungu Aliye juu ni mkombozi wao. |
36. | Lakini walimdanganya kwa vinywa vyao, Wakamwambia uongo kwa ndimi zao. |
37. | Kwa maana mioyo yao haikuwa thabiti kwake, Wala hawakuwa waaminifu katika agano lake. |
38. | Lakini Yeye, kwa kuwa anayo rehema, Husamehe uovu wala haangamizi. Mara nyingi huipishia mbali ghadhabu yake, Wala haiwashi hasira yake yote. |
39. | Akakumbuka ya kuwa wao ni kiwiliwili, Upepo upitao wala haurudi. |
40. | Walimwasi jangwani mara ngapi? Na kumhuzunisha nyikani! |
41. | Wakarudi nyuma wakamjaribu Mungu; Wakampa mpaka Mtakatifu wa Israeli. |
42. | Hawakuukumbuka mkono wake, Wala siku ile alipowakomboa na mtesi. |
43. | Alivyoziweka ishara zake katika Misri, Na miujiza yake katika konde la Soani. |
44. | Aligeuza damu mito yao, Na vijito wasipate kunywa. |
45. | Aliwapelekea mainzi wakawala, Na vyura wakawaharibu. |
46. | Akawapa tunutu mazao yao, Na nzige kazi yao. |
47. | Aliiharibu mizabibu yao kwa mvua ya mawe, Na mikuyu yao kwa mawe ya barafu. |
48. | Akaacha ng'ombe zao wapigwe kwa mvua ya mawe, Na makundi yao kwa umeme. |
49. | Akawapelekea ukali wa hasira yake, Ghadhabu, na uchungu, na taabu, Kundi la malaika waletao mabaya. |
50. | Akiifanyizia njia hasira yake; Wala hakuziepusha roho zao na mauti, Bali aliiachia tauni uhai wao; |
51. | Akampiga kila mzaliwa wa kwanza wa Misri, Malimbuko ya nguvu katika hema za Hamu. |
52. | Bali aliwaongoza watu wake kama kondoo, Akawachunga kama kundi jangwani. |
53. | Hao akawachukua salama wala hawakuogopa, Bali bahari iliwafunikiza adui zao. |
54. | Akawapeleka hadi mpaka wake mtakatifu, Mlima alioununua kwa mkono wake wa kuume. |
55. | Akawafukuza mataifa mbele yao, Akawapimia urithi kwa kamba, Na kuwakalisha kabila za Israeli katika hema zao. |
56. | Lakini walimjaribu Mungu Aliye juu, wakamwasi, Wala hawakuzishika shuhuda zake. |
57. | Bali walirudi nyuma, wakahaini kama baba zao; Wakaepea kama upinde usiofaa. |
58. | Wakamkasirisha kwa mahali pao pa juu, Wakamtia wivu kwa sanamu zao. |
59. | Mungu akasikia, akaghadhibika, Akamkataa Israeli kabisa. |
60. | Akaiacha maskani ya Shilo, Hema aliyoiweka katikati ya wanadamu; |
61. | Akaziacha nguvu zake kutekwa, Na fahari yake mkononi mwa mtesi. |
62. | Akawatoa watu wake wapigwe kwa upanga; Akaughadhibikia urithi wake. |
63. | Moto ukawala vijana wao, Wanawali wao hawakuimbiwa nyimbo za arusi, |
64. | Makuhani wao walianguka kwa upanga, Wala wajane wao hawakuomboleza. |
65. | Ndipo Bwana alipoamka kama aliyelala usingizi, Kama shujaa apigaye kelele sababu ya mvinyo; |
66. | Akawapiga watesi wake akawarudisha nyuma, Akawatia aibu ya milele. |
67. | Ila akaikataa hema ya Yusufu; Wala hakuichagua kabila ya Efraimu. |
68. | Bali aliichagua kabila ya Yuda, Mlima Sayuni alioupenda. |
69. | Akajenga patakatifu pake kama vilele, Kama dunia aliyoiweka imara milele. |
70. | Akamchagua Daudi, mtumishi wake, Akamwondoa katika mazizi ya kondoo. |
71. | Nyuma ya kondoo wanyonyeshao alimwondoa, Awachunge Yakobo watu wake, na Israeli urithi wake. |
72. | Akawalisha kwa ukamilifu wa moyo wake, Na kuwaongoza kwa busara ya mikono yake. |
← Psalms (78/150) → |