| ← Psalms (77/150) → |
| 1. | Nimpazie Mungu sauti yangu, Naam, nimpazie Mungu, naye atanisikia. |
| 2. | Siku ya taabu yangu nalimtafuta Bwana; Mkono wangu ulinyoshwa usiku, haukulegea; Nafsi yangu ilikataa kufarijika. |
| 3. | Nilipotaka kumkumbuka Mungu nalifadhaika; Nilipotaka kutafakari roho yangu ilizimia. |
| 4. | Ulizishika kope za macho yangu zisifumbike; Naliona mashaka nisiweze kunena. |
| 5. | Nalifikiri habari za siku za kale, Miaka ya zamani zilizopita. |
| 6. | Nakumbuka wimbo wangu usiku, Nawaza moyoni mwangu, Roho yangu ikatafuta. |
| 7. | Je! Bwana atatupa milele na milele? Hatatenda fadhili tena kabisa? |
| 8. | Rehema zake zimekoma hata milele? Ahadi yake imekwisha hata vizazi vyote? |
| 9. | Mungu amesahau fadhili zake? Amezuia kwa hasira rehema zake? |
| 10. | Nikasema, Ndio udhaifu wangu huo; Lakini nitaikumbuka miaka ya mkono wa kuume wake Aliye juu. |
| 11. | Nitayakumbuka matendo ya Bwana; Naam, nitayakumbuka maajabu yako ya kale. |
| 12. | Pia nitaitafakari kazi yako yote; Nitaziwaza habari za matendo yako. |
| 13. | Ee Mungu, njia yako i katika utakatifu; Ni nani aliye mungu mkuu kama Mungu? |
| 14. | Wewe ndiwe Mungu ufanyaye maajabu; Uliudhihirisha uweza wako kati ya mataifa. |
| 15. | Kwa mkono wako umewakomboa watu wako, Wana wa Yakobo na Yusufu. |
| 16. | Ee Mungu, yale maji yalikuona, Yale maji yalikuona, yakaogopa. Vilindi vya maji navyo vikatetemeka, |
| 17. | Mawingu yakamwaga maji. Mbingu nazo zikatoa sauti, Mishale yako nayo ikatapakaa. |
| 18. | Sauti ya radi yako ikawa katika kisulisuli; Umeme uliuangaza ulimwengu. Nchi ilitetemeka na kutikisika; |
| 19. | Njia yako ilikuwa katika bahari. Na mapito yako yalikuwa katika maji makuu; Hatua zako hazikujulikana. |
| 20. | Uliwaongoza watu wako kama kundi, Kwa mkono wa Musa na Haruni. |
| ← Psalms (77/150) → |