← Psalms (76/150) → |
1. | Katika Yuda Mungu amejulikana, Katika Israeli jina lake ni kuu. |
2. | Kibanda chake pia kiko Salemu, Na maskani yake iko Sayuni. |
3. | Huko ndiko alikoivunja mishale ya uta, Ngao, na upanga, na zana za vita. |
4. | Wewe U mwenye fahari na adhama, Toka milima ya mateka. |
5. | Wametekwa wenye moyo thabiti; Wamelala usingizi; Wala hawakuiona mikono yao Watu wote walio hodari. |
6. | Kwa kukemea kwako, Ee Mungu wa Yakobo, Gari na farasi wameshikwa na usingizi mzito. |
7. | Wewe ndiwe utishaye, naam, Wewe; Naye ni nani awezaye kusimama ufanyapo hasira? |
8. | Toka mbinguni ulitangaza hukumu; Nchi iliogopa, ikakaa kimya. |
9. | Mungu aliposimama ili kuhukumu Na kuwaokoa wapole wa dunia wote pia. |
10. | Maana hasira ya binadamu itakusifu, Masalio ya hasira utajifunga kama mshipi. |
11. | Wekeni nadhiri, mkaziondoe Kwa Bwana, Mungu wenu. Wote wanaomzunguka wamletee hedaya, Yeye astahiliye kuogopwa. |
12. | Yeye huzikata roho za wakuu; Na kuwatisha wafalme wa dunia. |
← Psalms (76/150) → |