Psalms (75/150)  

1. Ee Mungu, twakushukuru. Twakushukuru kwa kuwa Jina lako li karibu; Watu huyasimulia matendo yako ya ajabu.
2. Nitakapoufikia wakati ulioamriwa, Mimi nitahukumu hukumu za haki.
3. Ingawa dunia na wote wakaao humo wataharuki, Mimi mwenyewe nimezisimamisha nguzo zake.
4. Naliwaambia waliojivuna, Msijivune; Na wasio haki, Msiiinue pembe.
5. Msiiinue pembe yenu juu, Wala msinene kwa shingo ya kiburi.
6. Maana siko mashariki wala magharibi, Wala nyikani itokako heshima.
7. Bali Mungu ndiye ahukumuye; Humdhili huyu na kumwinua huyu.
8. Maana mkononi mwa Bwana mna kikombe, Na mvinyo yake inatoka povu; Kumejaa machanganyiko; Naye huyamimina. Na sira zake wasio haki wa dunia Watazifyonza na kuzinywa.
9. Bali mimi nitatangaza matendo yako milele, Nitamwimbia Mungu wa Yakobo.
10. Pembe zote za wasio haki nitazikata, Na pembe za mwenye haki zitainuka.

  Psalms (75/150)