← Psalms (74/150) → |
1. | Ee Mungu, mbona umetutupa milele? Kwa nini hasira yako inatoka moshi Juu ya kondoo wa malisho yako? |
2. | Ulikumbuke kusanyiko lako, Ulilolinunua zamani. Ulilolikomboa liwe kabila ya urithi wako, Mlima Sayuni ulioufanya maskani yako. |
3. | Upainulie miguu yako palipoharibika milele; Adui ameufanya kila ubaya katika patakatifu. |
4. | Watesi wako wamenguruma kati ya kusanyiko lako; Wameweka bendera zao ziwe alama. |
5. | Wanaonekana kama watu wainuao mashoka, Waikate miti ya msituni. |
6. | Na sasa nakishi yake yote pia Wanaivunja-vunja kwa mashoka na nyundo. |
7. | Wamepatia moto patakatifu pako; Wamelinajisi kao la jina lako hata chini. |
8. | Walisema mioyoni mwao, Na tuwaangamize kabisa; Mahali penye mikutano ya Mungu Wamepachoma moto katika nchi pia. |
9. | Hatuzioni ishara zetu, wala sasa hakuna nabii, Wala kwetu hakuna ajuaye, hata lini? |
10. | Ee Mungu, mtesi atalaumu hata lini? Adui alidharau jina lako hata milele? |
11. | Mbona unaurudisha mkono wako, Naam, mkono wako wa kuume, Uutoe kifuani mwako, Ukawaangamize kabisa. |
12. | Lakini Mungu ni mfalme wangu tokea zamani, Afanyaye mambo ya wokovu katikati ya nchi. |
13. | Wewe umeipasua bahari kwa nguvu zako, Umevivunja vichwa vya nyangumi juu ya maji. |
14. | Wewe uliviseta vichwa vya lewiathani, Awe chakula cha watu wa jangwani. |
15. | Wewe ulitokeza chemchemi na kijito; Wewe ulikausha mito yenye maji sikuzote. |
16. | Mchana ni wako, usiku nao ni wako, Ndiwe uliyeufanya mwanga na jua. |
17. | Wewe uliiweka mipaka yote ya dunia, Kaskazi na kusi Wewe ulizitengeneza. |
18. | Ee Bwana, uyakumbuke hayo, adui amelaumu, Na watu wapumbavu wamelidharau jina lako. |
19. | Usimpe mnyama mkali nafsi ya hua wako; Usiusahau milele uhai wa watu wako walioonewa. |
20. | Ulitafakari agano; Maana mahali penye giza katika nchi Pamejaa makao ya ukatili. |
21. | Aliyeonewa asirejee ametiwa haya, Mnyonge na mhitaji na walisifu jina lako. |
22. | Ee Mungu, usimame, ujitetee mwenyewe, Ukumbuke unavyotukanwa na mpumbavu mchana kutwa. |
23. | Usiisahau sauti ya watesi wako, Ghasia yao wanaokuondokea inapaa daima. |
← Psalms (74/150) → |