| ← Psalms (73/150) → |
| 1. | Hakika Mungu ni mwema kwa Israeli, Kwa hao walio safi mioyo yao. |
| 2. | Nami miguu yangu ilikuwa karibu na kupotoka, Hatua zangu zilikuwa karibu na kuteleza. |
| 3. | Maana naliwaonea wivu wenye kujivuna, Nilipoiona hali ya amani ya wasio haki. |
| 4. | Maana hawana maumivu katika kufa kwao, Na mwili wao una nguvu. |
| 5. | Katika taabu ya watu hawamo, Wala hawapati mapigo pamoja na wanadamu. |
| 6. | Hivyo kiburi kimekuwa mkufu shingoni mwao, Jeuri huwavika kama nguo. |
| 7. | Macho yao hutokeza kwa kunenepa, Wameipita kadiri ya mawazo ya mioyo yao. |
| 8. | Hudhihaki, husimulia mabaya, Husimulia udhalimu kana kwamba wako juu. |
| 9. | Wameweka kinywa chao mbinguni, Na ulimi wao hutanga-tanga duniani. |
| 10. | Kwa hiyo watu wake hugeuka huko, Na maji yaliyojaa humezwa nao. |
| 11. | Nao husema, Mungu ajuaje? Yako maarifa kwake aliye juu? |
| 12. | Fahamu, ndivyo walivyo wasio haki, Na kwa kustarehe sikuzote wamepata mali nyingi. |
| 13. | Hakika nimejisafisha moyo wangu bure, Nimenawa mikono yangu kwa kutokukosa. |
| 14. | Maana mchana kutwa nimepigwa, Na kuadhibiwa kila asubuhi. |
| 15. | Kama ningalisema, Nitasimulia kama hayo; Kumbe! Ningaliwadanganya kizazi cha wana wako. |
| 16. | Nami nalifikiri jinsi ya kufahamu hayo; Ikawa taabu machoni pangu; |
| 17. | Hata nilipoingia katika patakatifu pa Mungu, Nikautafakari mwisho wao. |
| 18. | Hakika Wewe huwaweka penye utelezi, Huwaangusha mpaka palipoharibika. |
| 19. | Namna gani wamekuwa ukiwa mara! Wametokomea na kutoweshwa kwa utisho. |
| 20. | Ee Bwana, kama ndoto wakati wa kuamka, Uondokapo utaidharau sanamu yao. |
| 21. | Moyo wangu ulipoona uchungu, Viuno vyangu viliponichoma, |
| 22. | Nalikuwa kama mjinga, sijui neno; Nalikuwa kama mnyama tu mbele zako. |
| 23. | Walakini mimi ni pamoja nawe daima, Umenishika mkono wa kuume. |
| 24. | Utaniongoza kwa shauri lako, Na baadaye utanikaribisha kwa utukufu. |
| 25. | Ni nani niliye naye mbinguni, Wala duniani sina cha kupendeza ila Wewe. |
| 26. | Mwili wangu na moyo wangu hupunguka, Bali Mungu ni mwamba wa moyo wangu Na sehemu yangu milele. |
| 27. | Maana wajitengao nawe watapotea; Umewaangamiza wote waliokuacha Wewe. |
| 28. | Nami kumkaribia Mungu ni kwema kwangu; Nimefanya kimbilio kwa Bwana MUNGU, Niyahubiri matendo yako yote. |
| ← Psalms (73/150) → |