| ← Psalms (71/150) → |
| 1. | Nimekukimbilia Wewe, Bwana, Nisiaibike milele. |
| 2. | Kwa haki yako uniponye, uniopoe, Unitegee sikio lako, uniokoe. |
| 3. | Uwe kwangu mwamba wa makazi yangu, Nitakakokwenda sikuzote. Umeamuru niokolewe, Ndiwe genge langu na ngome yangu. |
| 4. | Ee Mungu wangu, uniopoe mkononi mwa mkorofi, Katika mkono wake mwovu, mdhalimu, |
| 5. | Maana ndiwe taraja langu, Ee Bwana MUNGU, Tumaini langu tokea ujana wangu. |
| 6. | Nimekutegemea Wewe tangu kuzaliwa, Ndiwe uliyenitoa tumboni mwa mama yangu, Ninakusifu Wewe daima. |
| 7. | Nimekuwa kitu cha ajabu kwa watu wengi, Na Wewe ndiwe kimbilio langu la nguvu. |
| 8. | Kinywa changu kitajazwa sifa zako, Na heshima yako mchana kutwa. |
| 9. | Usinitupe wakati wa uzee, Nguvu zangu zipungukapo usiniache. |
| 10. | Kwa maana adui zangu wananiamba, Nao wanaoniotea roho yangu hushauriana. |
| 11. | Wakisema, Mungu amemwacha, Mfuatieni, mkamateni, hakuna wa kumponya. |
| 12. | Ee Mungu, usiwe mbali nami; Ee Mungu wangu, fanya haraka kunisaidia. |
| 13. | Waaibishwe, watoweshwe, adui za nafsi yangu. Wavikwe laumu na aibu wanaonitakia mabaya. |
| 14. | Nami nitatumaini daima, Nitazidi kuongeza sifa zake zote. |
| 15. | Kinywa changu kitasimulia haki na wokovu wako Mchana kutwa; maana sijui hesabu yake. |
| 16. | Nitakuja na mambo ya ajabu ya Bwana MUNGU; Nitawakumbusha watu haki yako Wewe peke yako. |
| 17. | Ee Mungu, umenifundisha tokea ujana wangu; Nimekuwa nikitangaza miujiza yako hata leo. |
| 18. | Na hata nikiwa ni mzee mwenye mvi, Ee Mungu, usiniache. Hata niwaeleze watu wa kizazi hiki nguvu zako, Na kila atakayekuja uweza wako. |
| 19. | Na haki yako, Ee Mungu, Imefika juu sana. Wewe uliyefanya mambo makuu; Ee Mungu, ni nani aliye kama Wewe? |
| 20. | Wewe, uliyetuonyesha mateso mengi, mabaya, Utatuhuisha tena. Utatupandisha juu tena Tokea pande za chini ya nchi. |
| 21. | Laiti ungeniongezea ukuu! Urejee tena na kunifariji moyo. |
| 22. | Nami nitakushukuru kwa kinanda, Na kweli yako, Ee Mungu wangu. Nitakuimbia Wewe kwa kinubi, Ee Mtakatifu wa Israeli. |
| 23. | Midomo yangu itafurahi sana nikuimbiapo, Na nafsi yangu uliyoikomboa. |
| 24. | Ulimi wangu nao utasimulia Haki yako mchana kutwa. Kwa maana wameaibishwa, Wametahayarika, wanaonitakia mabaya. |
| ← Psalms (71/150) → |