| ← Psalms (7/150) → |
| 1. | Bwana, Mungu wangu, nimekukimbilia Wewe, Uniokoe na wote wanaonifuatia, uniponye. |
| 2. | Asije akaipapura nafsi yangu kama simba, Akiivunja-vunja pasipokuwa na wa kuponya. |
| 3. | Bwana, Mungu wangu, ikiwa nimetenda haya, Ikiwa mna uovu mikononi mwangu, |
| 4. | Ikiwa nimemlipa mabaya Yeye aliyekaa kwangu salama; (Hasha! Nimemponya yeye Aliyekuwa mtesi wangu bila sababu;) |
| 5. | Basi adui na anifuatie, Na kuikamata nafsi yangu; Naam, aukanyage uzima wangu, Na kuulaza utukufu wangu mavumbini. |
| 6. | Bwana uondoke kwa hasira yako; Ujiinue juu ya jeuri ya watesi wangu; Uamke kwa ajili yangu; Umeamuru hukumu. |
| 7. | Kusanyiko la mataifa na likuzunguke, Na juu yake uketi utawale. |
| 8. | Bwana atawaamua mataifa, Bwana, unihukumu mimi, Kwa kadiri ya haki yangu, Sawasawa na unyofu nilio nao. |
| 9. | Ubaya wao wasio haki na ukome, Lakini umthibitishe mwenye haki. Kwa maana mjaribu mioyo na viuno Ndiye Mungu aliye mwenye haki. |
| 10. | Ngao yangu ina Mungu, Awaokoaye wanyofu wa moyo. |
| 11. | Mungu ni mwamuzi mwenye haki, Naam, Mungu aghadhibikaye kila siku. |
| 12. | Mtu asiporejea ataunoa upanga wake; Ameupinda uta wake na kuuweka tayari; |
| 13. | Naye amemtengenezea silaha za kufisha, Akifanya mishale yake kuwa ya moto. |
| 14. | Tazama, huyu ana utungu wa uovu, Amechukua mimba ya madhara, amezaa uongo. |
| 15. | Amechimba shimo, amelichimba chini sana, Akatumbukia katika handaki aliyoifanya! |
| 16. | Madhara yake yatamrejea kichwani pake, Na dhuluma yake itamshukia utosini. |
| 17. | Nitamshukuru Bwana kwa kadiri ya haki yake; Nitaliimbia jina la Bwana aliye juu. |
| ← Psalms (7/150) → |