Psalms (69/150)  

1. Ee Mungu, uniokoe, Maana maji yamefika mpaka nafsini mwangu.
2. Ninazama katika matope mengi, Pasipowezekana kusimama. Nimefika penye maji ya vilindi, Mkondo wa maji unanigharikisha.
3. Nimechoka kwa kulia kwangu, Koo yangu imekauka. Macho yangu yamedhoofu Kwa kumngoja Mungu wangu.
4. Wanaonichukia bure ni wengi Kuliko nywele za kichwa changu. Watakao kunikatilia mbali wamekuwa hodari, Adui zangu kwa sababu isiyo kweli. Hata mimi nalilipishwa kwa nguvu Vitu nisivyovichukua.
5. Ee Mungu, unajua upumbavu wangu, Wala hukufichwa dhambi yangu.
6. Wanaokungoja Wewe wasiaibishwe, Kwa ajili yangu, Bwana, MUNGU wa majeshi. Wanaokutafuta Wewe wasifedheheshwe, Kwa ajili yangu, Ee Mungu wa Israeli.
7. Maana kwa ajili yako nimestahimili laumu, Fedheha imenifunika uso wangu.
8. Nimekuwa mgeni kwa ndugu zangu, Na msikwao kwa wana wa mama yangu.
9. Maana wivu wa nyumba yako umenila, Na laumu zao wanaokulaumu zimenipata.
10. Nilipolia na kuiadhibu roho yangu kwa kufunga, Ikawa laumu juu yangu.
11. Nilipofanya gunia kuwa nguo zangu, Nikawa mithali kwao.
12. Waketio langoni hunisema, Na nyimbo za walevi hunidhihaki.
13. Nami maombi yangu nakuomba Wewe, Bwana, Wakati ukupendezao; Ee Mungu, Kwa wingi wa fadhili zako unijibu, Katika kweli ya wokovu wako.
14. Uniponye kwa kunitoa matopeni, Wala usiniache nikazama. Na niponywe nao wanaonichukia, Na katika vilindi vya maji.
15. Mkondo usinigharikishe, wala vilindi visinimeze, Wala shimo lisifumbe kinywa chake juu yangu.
16. Ee Bwana, unijibu, maana fadhili zako ni njema, Kwa kadiri ya rehema zako unielekee.
17. Wala usinifiche uso wako, mimi mtumishi wako, Maana mimi nimo taabuni, unijibu upesi.
18. Uikaribie nafsi yangu, uikomboe, Kwa sababu ya adui zangu unifidie.
19. Wewe umejua kulaumiwa kwangu, Na kuaibika na kufedheheka kwangu, Mbele zako Wewe wako watesi wangu wote.
20. Laumu imenivunja moyo, Nami ninaugua sana. Nikangoja aje wa kunihurumia, wala hakuna; Na wa kunifariji, wala sikumwona mtu.
21. Wakanipa uchungu kuwa chakula changu; Nami nilipokuwa na kiu wakaninywesha siki.
22. Meza yao mbele yao na iwe mtego; Naam, wakiwa salama na iwe tanzi.
23. Macho yao yatiwe giza wasione, Na viuno vyao uvitetemeshe daima.
24. Uimwage ghadhabu yako juu yao, Na ukali wa hasira yako uwapate.
25. Matuo yao na yawe ukiwa, Pasiwe na mtu wa kukaa hemani mwao.
26. Maana wanamwudhi mtu uliyempiga Wewe, Wanasimulia maumivu ya hao uliowatia jeraha.
27. Uwaongezee uovu juu ya uovu, Wala wasiingie katika haki yako.
28. Na wafutwe katika chuo cha uhai, Wala pamoja na wenye haki wasiandikwe.
29. Nami niliye maskini na mtu wa huzuni, Mungu, wokovu wako utaniinua.
30. Nitalisifu jina la Mungu kwa wimbo, Nami nitamtukuza kwa shukrani.
31. Nayo yatampendeza Bwana kuliko ng'ombe, Au ndama mwenye pembe na kwato.
32. Walioonewa watakapoona watafurahi; Enyi mmtafutao Mungu, mioyo yenu ihuishwe.
33. Kwa kuwa Bwana huwasikia wahitaji, Wala hawadharau wafungwa wake.
34. Mbingu na nchi zimsifu, Bahari na vyote viendavyo ndani yake.
35. Maana Mungu ataiokoa Sayuni, na kuijenga miji ya Yuda, Na watu watakaa ndani yake na kuimiliki.
36. Wazao wa watumishi wake watairithi, Nao walipendao jina lake watakaa humo.

  Psalms (69/150)