← Psalms (68/150) → |
1. | Mungu huondoka, adui zake wakatawanyika, Nao wamchukiao huukimbia uso wake. |
2. | Kama moshi upeperushwavyo, Ndivyo uwapeperushavyo wao; Kama nta iyeyukavyo mbele ya moto, Ndivyo waovu wapoteavyo usoni pa Mungu. |
3. | Bali wenye haki hufurahi, Na kuushangilia uso wa Mungu, Naam, hupiga kelele kwa furaha. |
4. | Mwimbieni Mungu, lisifuni jina lake, Mtengenezeeni njia ya barabara, Apitaye majangwani kama mpanda farasi; Jina lake ni YAHU; shangilieni mbele zake. |
5. | Baba wa yatima na mwamuzi wa wajane, Mungu katika kao lake takatifu. |
6. | Mungu huwakalisha wapweke nyumbani; Huwatoa wafungwa wakae hali ya kufanikiwa; Bali wakaidi hukaa katika nchi kavu. |
7. | Ee Mungu, ulipotoka mbele ya watu wako, Ulipopita nyikani, |
8. | Nchi ilitetemeka Naam, mbingu zilidondoka usoni pa Mungu; Hata Sinai usoni pa Mungu; Mungu wa Israeli. |
9. | Ee Mungu, ulinyesha mvua ya neema; Urithi wako ulipochoka uliutia nguvu. |
10. | Kabila yako ilifanya kao lake huko; Ee Mungu, kwa wema wako uliwaruzuku walioonewa. |
11. | Bwana analitoa neno lake; Wanawake watangazao habari ni jeshi kubwa; |
12. | Wafalme wa majeshi wanakimbia, wanakimbia; Na mwanamke akaaye nyumbani agawa nyara. |
13. | Kwa nini kulala mazizini arukapo hua, Mbawa zake ziking'aa kama fedha Na manyoya yake kama dhahabu? |
14. | Mwenyezi Mungu alipotawanya wafalme huko, Kulinyesha theluji katika Salmoni. |
15. | Ni mlima wa Mungu mlima Bashani, Ni mlima mrefu mlima Bashani. |
16. | Enyi milima mirefu, kwani kuutazama kwa wivu Mlima alioutamani Mungu akae juu yake? Naam, Bwana atakaa juu yake milele. |
17. | Magari ya Mungu ni ishirini elfu, maelfu maelfu; Bwana yumo kati yao kama katika Sinai, Katika patakatifu. |
18. | Wewe umepaa juu, umeteka mateka, Umepewa vipawa katikati ya wanadamu; Naam, hata na wakaidi, Bwana Mungu akae nao. |
19. | Na ahimidiwe Bwana, Siku kwa siku hutuchukulia mzigo wetu; Mungu ndiye wokovu wetu. |
20. | Mungu kwetu sisi ni Mungu wa kuokoa; Na njia za kutoka mautini zina YEHOVA Bwana. |
21. | Naam, Mungu atakipasua kichwa cha adui zake, Utosi wenye nywele wa mtu afulizaye kukosa. |
22. | Bwana alisema, Kutoka Bashani nitawarudisha, Nitawarudisha kutoka vilindi vya bahari; |
23. | Uuchovye mguu wako katika damu ya adui zako, Na ulimi wa mbwa zako upate sehemu yake. |
24. | Ee Mungu, wameiona miendo yako; Miendo ya Mungu wangu, Mfalme wangu, katika patakatifu |
25. | Waimbaji hutangulia, nyuma yao wapigao vinanda, Kati ya wanawali wapiga matari. |
26. | Mhimidini Mungu katika mikutano, Bwana katika makusanyiko ya Israeli. |
27. | Yuko Benyamini mdogo, mtawala wao; Wakuu wa Yuda, kundi lao; Wakuu wa Zabuloni; Wakuu wa Naftali. |
28. | Ee Mungu, uziamuru nguvu zako; Ee Mungu, uwe hodari uliyetufanyia makuu. |
29. | Kwa ajili ya hekalu lako Yerusalemu Wafalme watakuletea hedaya. |
30. | Mkemee mnyama wa manyasini; Kundi la mafahali, na ndama za watu; Hata wanyenyekee na kuleta vipande vya fedha, Uwatawanye watu wapendao vita. |
31. | Masheki watakuja kutoka Misri, Kushi itamnyoshea Mungu mikono yake mara. |
32. | Enyi falme za dunia, mwimbieni Mungu, Msifuni Bwana kwa nyimbo. |
33. | Apandaye mbingu za mbingu za tangu milele; Aitoa sauti yake, sauti ya nguvu. |
34. | Mhesabieni Mungu nguvu; Enzi yake i juu ya Israeli; Na nguvu zake zi mawinguni. |
35. | Mungu ni mwenye kutisha Kutoka patakatifu pako. Ndiye Mungu wa Israeli; Yeye huwapa watu wake nguvu na uwezo. Na ahimidiwe Mungu. |
← Psalms (68/150) → |