← Psalms (66/150) → |
1. | Mpigie Mungu kelele za shangwe, nchi yote, |
2. | Imbeni utukufu wa jina lake, Tukuzeni sifa zake. |
3. | Mwambieni Mungu, Matendo yako yatisha kama nini! Kwa ajili ya wingi wa nguvu zako, Adui zako watakuja kunyenyekea mbele zako. |
4. | Nchi yote itakusujudia na kukuimbia, Naam, italiimbia jina lako. |
5. | Njoni yatazameni matendo ya Mungu; Hutisha kwa mambo awatendayo wanadamu; |
6. | Aligeuza bahari ikawa nchi kavu; Katika mto walivuka kwa miguu; Huko ndiko mlikomfurahia. |
7. | Atawala kwa uweza wake milele; Macho yake yanaangalia mataifa; Waasio wasijitukuze nafsi zao. |
8. | Enyi mataifa, mtukuzeni Mungu wetu, Itangazeni sauti ya sifa zake; |
9. | Aliyeiweka nafsi yetu katika uhai, Wala hakuuacha mguu wetu usogezwe. |
10. | Kwa maana umetupima, Ee Mungu, Umetujaribu inavyojaribiwa fedha. |
11. | Ulituingiza ndani ya wavu, Na kuweka viunoni mwetu mzigo uliotulemea. |
12. | Uliwapandisha watu Juu ya vichwa vyetu. Tulipita motoni na majini; Ukatutoa na kutuleta kunako wingi. |
13. | Nitaingia nyumbani mwako na kafara; Nitaondoa kwako nadhiri zangu; |
14. | Ambazo midomo yangu ilizinena; Kinywa changu kikazisema nilipokuwa taabuni. |
15. | Kafara za vinono nitakutolea, Pamoja na fukizo la kondoo waume, Nitatoa ng'ombe pamoja na mbuzi. |
16. | Njoni, sikieni, ninyi nyote mnaomcha Mungu, Nami nitayatangaza aliyonitendea roho yangu. |
17. | Nalimwita kwa kinywa changu, Na sifa kuu zilikuwa chini ya ulimi wangu. |
18. | Kama ningaliwaza maovu moyoni mwangu, Bwana asingesikia. |
19. | Hakika Mungu amesikia; Ameisikiliza sauti ya maombi yangu. |
20. | Na ahimidiwe Mungu asiyeyakataa maombi yangu, Wala kuniondolea fadhili zake. |
← Psalms (66/150) → |