Psalms (65/150)  

1. Ee Mungu, sifa zakulaiki katika Sayuni, Na kwako Wewe itaondolewa nadhiri.
2. Wewe usikiaye kuomba, Wote wenye mwili watakujia.
3. Ingawa maovu mengi yanamshinda, Wewe utayafunika maasi yetu.
4. Heri mtu yule umchaguaye, Na kumkaribisha akae nyuani mwako. Na tushibe wema wa nyumba yako, Patakatifu pa hekalu lako.
5. Kwa mambo ya kutisha utatujibu, Katika haki, Ee Mungu wa wokovu wetu. Wewe uliye tumaini la miisho yote ya dunia, Na la bahari iliyo mbali sana,
6. Milima waiweka imara kwa nguvu zako, Huku ukijifunga uweza kama mshipi.
7. Wautuliza uvumi wa bahari, Uvumi wa mawimbi yake, Na ghasia ya mataifa;
8. Kwa hiyo wakaao mbali kabisa huogopa ishara zako; Milango ya asubuhi na jioni waifurahisha.
9. Umeijilia nchi na kuisitawisha, Umeitajirisha sana; Mto wa Mungu umejaa maji; Wawaruzuku watu nafaka Maana ndiwe uitengenezaye ardhi.
10. Matuta yake wayajaza maji; Wapasawazisha palipoinuka, Wailainisha nchi kwa manyunyu; Waibariki mimea yake.
11. Umeuvika mwaka taji ya wema wako; Mapito yako yadondoza unono.
12. Huyadondokea malisho ya nyikani, Na vilima vyajifunga furaha.
13. Na malisho yamevikwa kondoo, Na mabonde yamepambwa nafaka, Yanashangilia, naam, yanaimba.

  Psalms (65/150)