Psalms (58/150)  

1. Ni kweli, enyi wakuu, mnanena haki? Enyi wanadamu, mnahukumu kwa adili?
2. Sivyo! Mioyoni mwenu mnatenda maovu; Katika nchi mnapima udhalimu wa mikono yenu.
3. Wasio haki wamejitenga tangu kuzaliwa kwao; Tangu tumboni wamepotea, wakisema uongo.
4. Sumu yao, mfano wake ni sumu ya nyoka; Mfano wao ni fira kiziwi azibaye sikio lake.
5. Asiyeisikiliza sauti ya waganga, Ijapo wanafanya uganga kwa ustadi.
6. Ee Mungu, uyavunje meno yao vinywani mwao; Ee Bwana, uyavunje magego ya wana-simba.
7. Na watoweke kama maji yapitayo kwa kasi; Akiielekeza mishale yake, iwe imetiwa ubutu.
8. Kama konokono ayeyukaye na kutoweka, Kama mimba iliyoharibika, isiyoliona jua,
9. Kabla ya masufuria yenu kupata moto wa miiba, Ataipeperusha kama chamchela, Iliyo mibichi na iliyo moto.
10. Mwenye haki atafurahi akionapo kisasi; Ataiosha miguu yake katika damu ya wasio haki.
11. Na mwanadamu atasema, Hakika iko thawabu yake mwenye haki. Hakika yuko Mungu Anayehukumu katika dunia.

  Psalms (58/150)