Psalms (56/150)  

1. Mungu, unirehemu, maana yuko atakaye kunimeza, Mchana kutwa ananionea akileta vita.
2. Adui zangu wanataka kunimeza mchana kutwa, Maana waletao vita juu yangu kwa kiburi ni wengi.
3. Siku ya hofu yangu nitakutumaini Wewe;
4. Kwa msaada wa MUNGU nitalisifu neno lake. Nimemtumaini Mungu, sitaogopa; Mwenye mwili atanitenda nini?
5. Mchana kutwa wanapotosha maneno yangu, Mawazo yao yote ni juu yangu kunitakia mabaya.
6. Hukutanika, hujificha, huziangalia nyayo zangu, Kwa kuwa wameniotea nafsi yangu.
7. Je! Wataokoka kwa uovu wao? Ee Mungu, uwaangamize kwa hasira yako.
8. Umehesabu kutanga-tanga kwangu; Uyatie machozi yangu katika chupa yako; (Je! Hayamo katika kitabu chako?)
9. Ndipo adui zangu watarudi nyuma siku ile niitapo. Neno hili najua kuwa MUNGU yu upande wangu;
10. Kwa msaada wa MUNGU nitalisifu neno lake. Kwa msaada wa Bwana nitalisifu neno lake.
11. Nimemtumaini Mungu, sitaogopa; Mwanadamu atanitenda nini?
12. Ee Mungu, nadhiri zako zi juu yangu; Nitakutolea dhabihu za kushukuru.
13. Maana umeniponya nafsi yangu na mauti; Je! Hukuizuia miguu yangu isianguke? Ili nienende mbele za Mungu Katika nuru ya walio hai.

  Psalms (56/150)