← Psalms (55/150) → |
1. | Ee Mungu, uisikilize sala yangu, Wala usijifiche nikuombapo rehema. |
2. | Unisikilize na kunijibu, Nimetanga-tanga nikilalama na kuugua. |
3. | Kwa sababu ya sauti ya adui, Kwa sababu ya dhuluma yake yule mwovu. Kwa maana wananitupia uovu, Na kwa ghadhabu wananiudhi. |
4. | Moyo wangu unaumia ndani yangu, Na hofu za mauti zimeniangukia. |
5. | Hofu na tetemeko limenijia, Na hofu kubwa imenifunikiza. |
6. | Nikasema, Ningekuwa na mbawa kama njiwa, Ningerukia mbali na kustarehe. |
7. | Ningekwenda zangu mbali, Ningetua jangwani. |
8. | Ningefanya haraka kuzikimbia Dhoruba na tufani. |
9. | Ee Bwana, uwaangamize, uzichafue ndimi zao, Maana nimeona dhuluma na fitina katika mji. |
10. | Mchana na usiku huzunguka kutani mwake; Uovu na taabu zimo ndani yake; |
11. | Tamaa mbaya zimo ndani yake; Dhuluma na hila haziondoki mitaani mwake. |
12. | Kwa maana aliyetukana si adui; Kama ndivyo, ningevumilia. Aliyejitukuza juu yangu siye anichukiaye; Kama ndivyo, ningejificha asinione. |
13. | Bali ni wewe, mtu mwenzangu, Rafiki yangu, niliyejuana nawe sana. |
14. | Tulipeana shauri tamu; na kutembea Nyumbani mwa Mungu pamoja na mkutano. |
15. | Mauti na iwapate kwa ghafula, Na washuke kuzimu wangali hai, Maana uovu u makaoni mwao na katikati yao. |
16. | Nami nitamwita Mungu, Na Bwana ataniokoa; |
17. | Jioni, asubuhi, na adhuhuri nitalalama na kuugua, Naye ataisikia sauti yangu. |
18. | Ameiokoa nafsi yangu iwe salama, asinikaribie mtu, Maana walioshindana nami walikuwa wengi. |
19. | Mungu atasikia na kuwajibu; Ndiye Yeye akaaye tangu milele. Mageuzi ya mambo hayawapati hao, Kwa hiyo hawamchi Mungu. |
20. | Amenyosha mkono awadhuru waliopatana naye, Amelihalifu agano lake. |
21. | Kinywa chake ni laini kuliko siagi, Bali moyo wake ni vita. Maneno yake ni mororo kuliko mafuta, Bali hayo ni panga wazi. |
22. | Umtwike Bwana mzigo wako naye atakutegemeza, Hatamwacha mwenye haki aondoshwe milele. |
23. | Nawe, Ee Mungu, utawatelemsha, Walifikilie shimo la uharibifu; Watu wa damu na hila hawataishi nusu ya siku zao, Bali mimi nitakutumaini Wewe. |
← Psalms (55/150) → |