| ← Psalms (49/150) → |
| 1. | Sikieni haya, enyi mataifa yote; Sikilizeni, ninyi nyote mnaokaa duniani. |
| 2. | Watu wakuu na watu wadogo wote pia, Tajiri na maskini wote pamoja. |
| 3. | Kinywa changu kitanena hekima, Na fikira za moyo wangu zitakuwa za busara. |
| 4. | Nitatega sikio langu nisikie mithali, Na kufumbua fumbo langu kwa kinubi |
| 5. | Kwa nini niogope siku za uovu, Ubaya ukinizunguka miguuni pangu? |
| 6. | Wa hao wanaozitumainia mali zao, Na kujisifia wingi wa utajiri wao; |
| 7. | Hakuna mtu awezaye kumkomboa ndugu yake, Wala kumpa Mungu fidia kwa ajili yake, |
| 8. | (Maana fidia ya nafsi zao ina gharama, Wala hana budi kuiacha hata milele;) |
| 9. | ili aishi sikuzote asilione kaburi. |
| 10. | Naam, ataliona, hata wenye hekima hufa; Mpumbavu na mjinga hupotea pamoja, Na kuwaachia wengine mali zao. |
| 11. | Makaburi ni nyumba zao hata milele, Maskani zao vizazi hata vizazi. Hao waliotaja mashamba yao Kwa majina yao wenyewe. |
| 12. | Lakini mwanadamu hadumu katika heshima, Bali amefanana na wanyama wapoteao. |
| 13. | Hiyo ndiyo njia yao, ujinga wao, Nao walioko baada yao huyaridhia maneno yao. |
| 14. | Kama kondoo wamewekwa kwenda kuzimu, Na mauti itawachunga; Watu wanyofu watawamiliki asubuhi; Umbo lao litachakaa, kao lao ni kuzimu. |
| 15. | Bali Mungu atanikomboa nafsi yangu, Atanitoa mkononi mwa kuzimu, maana atanikaribisha. |
| 16. | Usiogope mtu atakapopata utajiri, Na fahari ya nyumba yake itakapozidi. |
| 17. | Maana atakapokufa hatachukua cho chote; Utukufu wake hautashuka ukimfuata. |
| 18. | Ajapojibariki nafsi yake alipokuwa hai, Na watu watakusifu ukijitendea mema, |
| 19. | Atakwenda kwenye kizazi cha baba zake Hawataona nuru hata milele. |
| 20. | Mwanadamu mwenye heshima, iwapo hana akili, Amefanana na wanyama wapoteao. |
| ← Psalms (49/150) → |