← Psalms (45/150) → |
1. | Moyo wangu umefurika kwa neno jema, Mimi nasema niliyomfanyizia mfalme; Ulimi wangu ni kalamu ya mwandishi mstadi. |
2. | Wewe u mzuri sana kuliko wanadamu; Neema imemiminiwa midomoni mwako, Kwa hiyo Mungu amekubariki hata milele. |
3. | Jifungie upanga wako pajani, wewe uliye hodari, Utukufu ni wako na fahari ni yako. |
4. | Katika fahari yako usitawi uendelee Kwa ajili ya kweli na upole na haki Na mkono wako wa kuume Utakufundisha mambo ya kutisha. |
5. | Mishale yako ni mikali, watu huanguka chini yako; Imo mioyoni mwa adui za mfalme. |
6. | Kiti chako cha enzi, Mungu, ni cha milele na milele, Fimbo ya ufalme wako ni fimbo ya adili. |
7. | Umeipenda haki; Umeichukia dhuluma. Kwa hiyo MUNGU, Mungu wako, amekupaka mafuta, Mafuta ya furaha kuliko wenzako. |
8. | Mavazi yako yote hunukia manemane Na udi na mdalasini. Katika majumba ya pembe Vinubi vimekufurahisha. |
9. | Binti za wafalme wamo Miongoni mwa akina bibi wako wastahiki. Mkono wako wa kuume amesimama malkia Amevaa dhahabu ya Ofiri. |
10. | Sikia, binti, utazame, utege sikio lako, Uwasahau watu wako na nyumba ya baba yako. |
11. | Naye mfalme atautamani uzuri wako, Maana ndiye bwana wako, nawe umsujudie. |
12. | Na binti Tiro analeta kipawa chake, Nao matajiri wa watu watajipendekeza kwako. |
13. | Binti mfalme yumo ndani ana fahari tupu, Mavazi yake ni ya nyuzi za dhahabu. |
14. | Atapelekwa kwa mfalme Na mavazi yaliyofumwa kwa uzuri. Wanawali wenzake wanaomfuata, Watapelekwa kwako. |
15. | Watapelekwa kwa furaha na shangwe, Na kuingia katika nyumba ya mfalme. |
16. | Badala ya baba zako watakuwapo watoto wako, Utawafanya kuwa wakuu katika nchi zote. |
17. | Jina lako nitalifanya kuwa kumbukumbu Katika vizazi vyote. Kwa hiyo mataifa watakushukuru Milele na milele. |
← Psalms (45/150) → |