← Psalms (44/150) → |
1. | Ee Mungu, tumesikia kwa masikio yetu Baba zetu wametuambia, Matendo uliyoyatenda siku zao, siku za kale. |
2. | Wewe kwa mkono wako uliwafukuza mataifa, Ukawakalisha wao. Wewe uliwatesa watu wa nchi, Ukawaeneza wao. |
3. | Maana si kwa upanga wao walivyoimiliki nchi, Wala si mkono wao uliowaokoa; Bali mkono wako wa kuume, naam, mkono wako, Na nuru ya uso wako, kwa kuwa uliwaridhia. |
4. | Ee Mungu, Wewe ndiwe mfalme wangu, Uagize mambo ya wokovu kwa Yakobo. |
5. | Kwa nguvu zako tutawaangusha watesi wetu; Kwa jina lako tutawakanyaga watupingao. |
6. | Maana sitautumainia upinde wangu, Wala upanga wangu hautaniokoa. |
7. | Bali Wewe ndiwe uliyetuokoa na watesi wetu; Na watuchukiao umewaaibisha. |
8. | Tumejisifia Mungu mchana kutwa, Na jina lako tutalishukuru milele. |
9. | Lakini umetutupa, umetufedhehesha, Wala hutoki na majeshi yetu. |
10. | Waturudisha nyuma tukampa mtesi kisogo, Na watuchukiao wanajipatia mateka. |
11. | Umetutoa kama kondoo tuwe chakula, Na kututawanya kati ya mataifa. |
12. | Wawauza watu wako bila kupata mali, Wala hukupata faida kwa thamani yao. |
13. | Umetufanya kuwa lawama kwa jirani zetu, Mzaha na dhihaka kwao wanaotuzunguka. |
14. | Umetufanya kuwa mithali kwa mataifa, Sababu ya kutikisa kichwa kwa watu wa nchi. |
15. | Mchana kutwa fedheha yangu i mbele yangu, Na haya ya uso wangu imenifunika, |
16. | Kwa sauti ya mwenye kulaumu na kukufuru, Kwa sababu ya adui na mjilipiza kisasi. |
17. | Haya yote yametupata, bali hatukukusahau, Wala hatukulihalifu agano lako. |
18. | Hatukuiacha mioyo yetu irudi nyuma, Wala hatua zetu hazikuiacha njia yako. |
19. | Hata utuponde katika kao la mbwa-mwitu, Na kutufunika kwa uvuli wa mauti. |
20. | Ikiwa tumelisahau jina la Mungu wetu, Au kumnyoshea mungu mgeni mikono yetu; |
21. | Je! Mungu hatalichunguza neno hilo? Maana ndiye azijuaye siri za moyo. |
22. | Hasha! Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa; Tunafanywa kondoo waendao kuchinjwa. |
23. | Amka, Bwana, mbona umelala? Ondoka, usitutupe kabisa. |
24. | Mbona unatuficha uso wako, Na kusahau kuonewa na kudhulumiwa kwetu? |
25. | Maana nafsi yetu imeinama mavumbini, Tumbo letu limegandamana na nchi. |
26. | Uondoke, uwe msaada wetu, Utukomboe kwa ajili ya fadhili zako. |
← Psalms (44/150) → |