← Psalms (40/150) → |
1. | Nalimngoja Bwana kwa saburi, Akaniinamia akakisikia kilio changu. |
2. | Akanipandisha toka shimo la uharibifu, Toka udongo wa utelezi; Akaisimamisha miguu yangu mwambani, Akaziimarisha hatua zangu. |
3. | Akatia wimbo mpya kinywani mwangu, Ndio sifa zake Mungu wetu. Wengi wataona na kuogopa, Nao watamtumaini Bwana |
4. | Heri aliyemfanya Bwana kuwa tumaini lake, Wala hakuwaelekea wenye kiburi, Wala hao wanaogeukia uongo. |
5. | Ee Bwana, Mungu wangu, umefanya kwa wingi Miujiza yako na mawazo yako kwetu; Hakuna awezaye kufananishwa nawe; Kama ningependa kuyatangaza na kuyahubiri, Ni mengi sana hayahesabiki. |
6. | Dhabihu na matoleo hukupendezwa nazo, Masikio yangu umeyazibua, Kafara na sadaka za dhambi hukuzitaka. |
7. | Ndipo niliposema, Tazama nimekuja, (Katika gombo la chuo nimeandikiwa,) |
8. | Kuyafanya mapenzi yako, Ee Mungu wangu, ndiyo furaha yangu; Naam, sheria yako imo moyoni mwangu. |
9. | Nimehubiri habari za haki katika kusanyiko kubwa. Sikuizuia midomo yangu; Ee Bwana, unajua. |
10. | Sikusitiri haki yako moyoni mwangu; Nimetangaza uaminifu wako na wokovu wako. Sikuficha fadhili zako wala kweli yako Katika kusanyiko kubwa. |
11. | Nawe, Bwana, usinizuilie rehema zako, Fadhili zako na kweli yako na zinihifadhi daima. |
12. | Kwa maana mabaya yasiyohesabika Yamenizunguka mimi. Maovu yangu yamenipata, Wala siwezi kuona. Yamezidi kuliko nywele za kichwa changu, Na moyo wangu umeniacha. |
13. | Ee Bwana, uwe radhi kuniokoa, Ee Bwana, unisaidie hima. |
14. | Waaibike, wafedheheke pamoja, Wanaoitafuta nafsi yangu waiangamize. Warudishwe nyuma, watahayarishwe, Wapendezwao na shari yangu. |
15. | Wakae hali ya ukiwa, na iwe aibu yao, Wanaoniambia, Ewe! Ewe! |
16. | Washangilie, wakufurahie, Wote wakutafutao. Waupendao wokovu wako Waseme daima, Atukuzwe Bwana. |
17. | Nami ni maskini na mhitaji, Bwana atanitunza. Ndiwe msaada wangu na mwokozi wangu, Ee Mungu wangu, usikawie. |
← Psalms (40/150) → |