← Psalms (39/150) → |
1. | Nalisema, Nitazitunza njia zangu Nisije nikakosa kwa ulimi wangu; Nitajitia lijamu kinywani, Maadamu mtu mbaya yupo mbele yangu. |
2. | Nalikuwa sisemi, nalinyamaa kimya, Sina faraja, maumivu yangu yakazidi. |
3. | Moyo wangu ukawa moto ndani yangu, Na katika kuwaza kwangu moto ukawaka; Nalisema kwa ulimi wangu, |
4. | Bwana, unijulishe mwisho wangu, Na kiasi cha siku zangu ni kiasi gani; Nijue jinsi nilivyo dhaifu. |
5. | Tazama, umefanya siku zangu kuwa mashubiri; Maisha yangu ni kama si kitu mbele zako. Kila mwanadamu, ingawa amesitawi, ni ubatili. |
6. | Binadamu huenda tu huko na huko kama kivuli; Hufanya ghasia tu kwa ajili ya ubatili; Huweka akiba wala hajui ni nani atakayeichukua. |
7. | Na sasa ninangoja nini, Ee Bwana? Matumaini yangu ni kwako. |
8. | Uniokoe na maasi yangu yote, Usinifanye laumu ya mpumbavu. |
9. | Nimenyamaza, sitafumbua kinywa changu, Maana Wewe ndiwe uliyeyafanya. |
10. | Uniondolee pigo lako; Kwa uadui wa mkono wako nimeangamia. |
11. | Ukimrudi mtu kwa kumkemea kwa uovu wake, Watowesha uzuri wake kama nondo. Kila mwanadamu ni ubatili. |
12. | Ee Bwana, usikie maombi yangu, Utege sikio lako niliapo, Usiyanyamalie machozi yangu. Kwa maana mimi ni mgeni wako, Msafiri kama baba zangu wote. |
13. | Uniachilie nikunjuke uso, Kabla sijaondoka nisiwepo tena. |
← Psalms (39/150) → |