| ← Psalms (38/150) → |
| 1. | Ee Bwana, usinilaumu katika ghadhabu yako, Wala usiniadhibu kwa ukali wa hasira yako. |
| 2. | Kwa maana mishale yako imenichoma, Na mkono wako umenipata. |
| 3. | Hamna uzima katika mwili wangu Kwa sababu ya ghadhabu yako. Wala hamna amani mifupani mwangu Kwa sababu ya hatia zangu. |
| 4. | Maana dhambi zangu zimenifunikiza kichwa, Kama mzigo mzito zimenilemea mno. |
| 5. | Jeraha zangu zinanuka, zimeoza, Kwa sababu ya upumbavu wangu. |
| 6. | Nimepindika na kuinama sana, Mchana kutwa nimekwenda nikihuzunika. |
| 7. | Maana viuno vyangu vimejaa homa, Wala hamna uzima katika mwili wangu. |
| 8. | Nimedhoofika na kuchubuka sana, Nimeugua kwa fadhaa ya moyo wangu. |
| 9. | Bwana, haja zangu zote ziko mbele zako, Kuugua kwangu hakukusitirika kwako. |
| 10. | Moyo wangu unapwita-pwita, Nguvu zangu zimeniacha; Nuru ya macho yangu nayo imeniondoka. |
| 11. | Wanipendao na rafiki zangu wanasimama mbali na pigo langu; Naam, karibu zangu wamesimama mbali. |
| 12. | Nao wanaoutafuta uhai wangu hutega mitego; Nao wanaotaka kunidhuru hunena mabaya; Na kufikiri hila mchana kutwa. |
| 13. | Lakini kama kiziwi sisikii, Nami ni kama bubu asiyefumbua kinywa chake. |
| 14. | Naam, nimekuwa kama mtu asiyesikia, Ambaye hamna hoja kinywani mwake. |
| 15. | Kwa kuwa nakungoja Wewe, Bwana, Wewe utajibu, Ee Bwana, Mungu wangu. |
| 16. | Maana nalisema, Wasije wakanifurahia; Mguu wangu ukiteleza wajitukuza juu yangu. |
| 17. | Kwa maana mimi ni karibu na kusita, Na maumivu yangu yako mbele yangu daima. |
| 18. | Kwa maana nitaungama uovu wangu, Na kusikitika kwa dhambi zangu. |
| 19. | Lakini adui zangu ni wazima wenye nguvu, Nao wanaonichukia bure wamekuwa wengi. |
| 20. | Naam, wakilipa mabaya kwa mema, Huwa adui zangu kwa kuwa nalifuata lililo jema. |
| 21. | Wewe, Bwana, usiniache, Mungu wangu, usijitenge nami. |
| 22. | Ufanye haraka kunisaidia, Ee Bwana, wokovu wangu. |
| ← Psalms (38/150) → |