← Psalms (37/150) → |
1. | Usikasirike kwa sababu ya watenda mabaya, Usiwahusudu wafanyao ubatili. |
2. | Maana kama majani watakatika mara, Kama miche mibichi watanyauka. |
3. | Umtumaini Bwana ukatende mema, Ukae katika nchi, upendezwe na uaminifu. |
4. | Nawe utajifurahisha kwa Bwana, Naye atakupa haja za moyo wako. |
5. | Umkabidhi Bwana njia yako, Pia umtumaini, naye atafanya. |
6. | Ataitokeza haki yako kama nuru, Na hukumu yako kama adhuhuri. |
7. | Ukae kimya mbele za Bwana, Nawe umngojee kwa saburi; Usimkasirikie yeye afanikiwaye katika njia yake, Wala mtu afanyaye hila. |
8. | Ukomeshe hasira, uache ghadhabu, Usikasirike, mwisho wake ni kutenda mabaya. |
9. | Maana watenda mabaya wataharibiwa, Bali wamngojao Bwana ndio watakaoirithi nchi. |
10. | Maana bado kitambo kidogo asiye haki hatakuwapo, Utapaangalia mahali pake wala hatakuwapo. |
11. | Bali wenye upole watairithi nchi, Watajifurahisha kwa wingi wa amani. |
12. | Asiye haki hunuia mabaya juu ya mwenye haki, Na kumsagia meno yake. |
13. | Bwana atamcheka, Maana ameona kwamba siku yake inakuja. |
14. | Wasio haki wamefuta upanga na kupinda uta, Wamwangushe chini maskini na mhitaji, Na kuwaua wenye mwenendo wa unyofu. |
15. | Upanga wao utaingia mioyoni mwao wenyewe, Na nyuta zao zitavunjika. |
16. | Kidogo alicho nacho mwenye haki ni bora Kuliko wingi wa mali wa wasio haki wengi. |
17. | Maana mikono ya wasio haki itavunjika, Bali Bwana huwategemeza wenye haki. |
18. | Bwana anazijua siku za wakamilifu, Na urithi wao utakuwa wa milele. |
19. | Hawataaibika wakati wa ubaya, Na siku za njaa watashiba. |
20. | Bali wasio haki watapotea, Nao wamchukiao Bwana watatoweka, Kama uzuri wa mashamba, Kama moshi watatoweka. |
21. | Asiye haki hukopa wala halipi, Bali mwenye haki hufadhili, hukirimu. |
22. | Maana waliobarikiwa na yeye watairithi nchi, Nao waliolaaniwa na yeye wataharibiwa. |
23. | Hatua za mtu zaimarishwa na Bwana, Naye aipenda njia yake. |
24. | Ajapojikwaa hataanguka chini, Bwana humshika mkono na kumtegemeza. |
25. | Nalikuwa kijana nami sasa ni mzee, Lakini sijamwona mwenye haki ameachwa Wala mzao wake akiomba chakula. |
26. | Mchana kutwa hufadhili na kukopesha, Na mzao wake hubarikiwa. |
27. | Jiepue na uovu, utende mema, Na kukaa hata milele. |
28. | Kwa kuwa Bwana hupenda haki, Wala hawaachi watauwa wake. Wao hulindwa milele, Bali mzao wa wasio haki ataharibiwa. |
29. | Wenye haki watairithi nchi, Nao watakaa humo milele. |
30. | Kinywa chake mwenye haki hunena hekima, Na ulimi wake husema hukumu. |
31. | Sheria ya Mungu wake imo moyoni mwake. Hatua zake hazitelezi. |
32. | Mtu asiye haki humvizia mwenye haki, Na kutafuta jinsi ya kumfisha. |
33. | Bwana hatamwacha mkononi mwake, Wala hatamlaumu atakapohukumiwa. |
34. | Wewe umngoje Bwana, Uishike njia yake, Naye atakutukuza uirithi nchi, Wasio haki watakapoharibiwa utawaona. |
35. | Nimemwona mtu asiye haki mkali sana, Akijieneza kama mwerezi wa Lebanoni. |
36. | Nikapita na kumbe! Hayuko, Nikamtafuta wala hakuonekana. |
37. | Umwangalie sana mtu mkamilifu, Umtazame mtu mnyofu, Maana mwisho wake mtu huyo ni amani. |
38. | Wakosaji wataangamizwa pamoja, Wasio haki mwisho wao wataharibiwa. |
39. | Na wokovu wa wenye haki una Bwana; Yeye ni ngome yao wakati wa taabu. |
40. | Naye Bwana huwasaidia na kuwaopoa; Huwaopoa na wasio haki na kuwaokoa; Kwa kuwa wamemtumaini Yeye. |
← Psalms (37/150) → |