| ← Psalms (33/150) → |
| 1. | Mpigieni Bwana vigelegele, enyi wenye haki, Kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo. |
| 2. | Mshukuruni Bwana kwa kinubi, Kwa kinanda cha nyuzi kumi mwimbieni sifa. |
| 3. | Mwimbieni wimbo mpya, Pigeni kwa ustadi kwa sauti ya shangwe. |
| 4. | Kwa kuwa neno la Bwana lina adili, Na kazi yake yote huitenda kwa uaminifu. |
| 5. | Huzipenda haki na hukumu, Nchi imejaa fadhili za Bwana. |
| 6. | Kwa neno la Bwana mbingu zilifanyika, Na jeshi lake lote kwa pumzi ya kinywa chake. |
| 7. | Hukusanya maji ya bahari chungu chungu, Huviweka vilindi katika ghala. |
| 8. | Nchi yote na imwogope Bwana, Wote wakaao duniani na wamche. |
| 9. | Maana Yeye alisema, ikawa; Na Yeye aliamuru, ikasimama. |
| 10. | Bwana huyabatilisha mashauri ya mataifa, Huyatangua makusudi ya watu. |
| 11. | Shauri la Bwana lasimama milele, Makusudi ya moyo wake vizazi na vizazi. |
| 12. | Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wao, Watu aliowachagua kuwa urithi wake. |
| 13. | Toka mbinguni Bwana huchungulia, Huwatazama wanadamu wote pia. |
| 14. | Toka mahali pake aketipo Huwaangalia wote wakaao duniani. |
| 15. | yeye aiumbaye mioyo yao wote Huzifikiri kazi zao zote. |
| 16. | Hapana mfalme aokokaye kwa wingi wa uwezo, Wala shujaa haokoki kwa wingi wa nguvu. |
| 17. | Farasi hafai kitu kwa wokovu, Wala hamponyi mtu kwa wingi wa nguvu zake. |
| 18. | Tazama, jicho la Bwana li kwao wamchao, Wazingojeao fadhili zake. |
| 19. | Yeye huwaponya nafsi zao na mauti, Na kuwahuisha wakati wa njaa. |
| 20. | Nafsi zetu zinamngoja Bwana; Yeye ndiye msaada wetu na ngao yetu. |
| 21. | Maana mioyo yetu itamfurahia, Kwa kuwa tumelitumainia jina lake takatifu. |
| 22. | Ee Bwana, fadhili zako zikae nasi, Kama vile tulivyokungoja Wewe. |
| ← Psalms (33/150) → |