| ← Psalms (31/150) → | 
| 1. | Nimekukimbilia Wewe, Bwana, Nisiaibike milele. Kwa haki yako uniponye, | 
| 2. | Unitegee sikio lako, uniokoe hima. Uwe kwangu mwamba wa nguvu, Nyumba yenye maboma ya kuniokoa. | 
| 3. | Ndiwe genge langu na ngome yangu; Kwa ajili ya jina lako uniongoze, unichunge. | 
| 4. | Utanitoa katika wavu walionitegea kwa siri, Maana Wewe ndiwe ngome yangu. | 
| 5. | Mikononi mwako naiweka roho yangu; Umenikomboa, Ee Bwana, Mungu wa kweli. | 
| 6. | Nawachukia wao washikao yasiyofaa yenye uongo; Bali mimi namtumaini Bwana. | 
| 7. | Na nishangilie, nizifurahie fadhili zako, Kwa kuwa umeyaona mateso yangu. Umeijua nafsi yangu taabuni, | 
| 8. | Wala hukunitia mikononi mwa adui; Miguu yangu umeisimamisha panapo nafasi. | 
| 9. | Ee Bwana, unifadhili, maana ni katika dhiki, Jicho langu limenyauka kwa masumbufu, Naam, mwili wangu na nafsi yangu. | 
| 10. | Maana maisha yangu yamekoma kwa huzuni, Na miaka yangu kwa kuugua. Nguvu zangu zinatetemeka kwa uovu wangu, Na mifupa yangu imekauka. | 
| 11. | Kwa sababu ya watesi wangu nimekuwa laumu, Naam, hasa kwa jirani zangu; Na kitu cha kutisha kwa rafiki zangu; Walioniona njiani walinikimbia. | 
| 12. | Nimesahauliwa kama mfu asiyekumbukwa; Nimekuwa kama chombo kilichovunjika. | 
| 13. | Maana nimesikia masingizio ya wengi; Hofu ziko pande zote. Waliposhauriana juu yangu, Walifanya hila wauondoe uhai wangu. | 
| 14. | Lakini mimi nakutumaini Wewe, Bwana, Nimesema, Wewe ndiwe Mungu wangu. | 
| 15. | Nyakati zangu zimo mikononi mwako; Uniponye na adui zangu, nao wanaonifuatia. | 
| 16. | Umwangaze mtumishi wako Kwa nuru ya uso wako; Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako. | 
| 17. | Ee Bwana, nisiaibishwe, maana nimekuita; Waaibishwe wasio haki, wanyamaze kuzimuni. | 
| 18. | Midomo ya uongo iwe na ububu, Imneneayo mwenye haki maneno ya kiburi, Kwa majivuno na dharau. | 
| 19. | Jinsi zilivyo nyingi fadhili zako Ulizowawekea wakuchao; Ulizowatendea wakukimbiliao Mbele ya wanadamu! | 
| 20. | Utawasitiri na fitina za watu Katika sitara ya kuwapo kwako; Utawaficha katika hema Na mashindano ya ndimi. | 
| 21. | Bwana ahimidiwe; kwa maana amenitendea Fadhili za ajabu katika mji wenye boma. | 
| 22. | Nami nalisema kwa haraka yangu, Nimekatiliwa mbali na macho yako; Lakini ulisikia sauti ya dua yangu Wakati nilipokulilia. | 
| 23. | Mpendeni Bwana, Ninyi nyote mlio watauwa wake. Bwana huwahifadhi waaminifu, Humlipa atendaye kiburi malipo tele. | 
| 24. | Iweni hodari, mpige moyo konde, Ninyi nyote mnaomngoja Bwana. | 
| ← Psalms (31/150) → |