← Psalms (27/150) → |
1. | Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu, Nimwogope nani? Bwana ni ngome ya uzima wangu, Nimhofu nani? |
2. | Watenda mabaya waliponikaribia, Wanile nyama yangu, Watesi wangu na adui zangu, Walijikwaa wakaanguka. |
3. | Jeshi lijapojipanga kupigana nami, Moyo wangu hautaogopa. Vita vijaponitokea, Hata hapo nitatumaini. |
4. | Neno Moja nimelitaka kwa Bwana, Nalo ndilo nitakalolitafuta, Nikae nyumbani mwa Bwana Siku zote za maisha yangu, Niutazame uzuri wa Bwana, Na kutafakari hekaluni mwake. |
5. | Mradi atanisitiri bandani mwake siku ya mabaya, Atanisitiri katika sitara ya hema yake, Na kuniinua juu ya mwamba. |
6. | Na sasa kichwa changu kitainuka Juu ya adui zangu wanaonizunguka. Nami nitatoa dhabihu za shangwe hemani mwake; Nitaimba, naam, nitamhimidi Bwana. |
7. | Ee Bwana, usikie, kwa sauti yangu ninalia, Unifadhili, unijibu. |
8. | Uliposema, Nitafuteni uso wangu, Moyo wangu umekuambia, Bwana, uso wako nitautafuta. |
9. | Usinifiche uso wako, Usijiepushe na mtumishi wako kwa hasira. Umekuwa msaada wangu, usinitupe, Wala usiniache, Ee Mungu wa wokovu wangu. |
10. | Baba yangu na mama yangu wameniacha, Bali Bwana atanikaribisha kwake. |
11. | Ee Bwana, unifundishe njia yako, Na kuniongoza katika njia iliyonyoka; Kwa sababu yao wanaoniotea; |
12. | Usinitie katika nia ya watesi wangu; Maana mashahidi wa uongo wameniondokea, Nao watoao jeuri kama pumzi. |
13. | Naamini ya kuwa nitauona wema wa Bwana Katika nchi ya walio hai. |
14. | Umngoje Bwana, uwe hodari, Upige moyo konde, naam, umngoje Bwana. |
← Psalms (27/150) → |