| ← Psalms (25/150) → |
| 1. | Ee Bwana, nakuinulia nafsi yangu, |
| 2. | Ee Mungu wangu, Nimekutumaini Wewe, nisiaibike, Adui zangu wasifurahi kwa kunishinda. |
| 3. | Naam, wakungojao hawataaibika hata mmoja; Wataaibika watendao uhaini bila sababu. |
| 4. | Ee Bwana, unijulishe njia zako, Unifundishe mapito yako, |
| 5. | Uniongoze katika kweli yako, Na kunifundisha. Maana Wewe ndiwe Mungu wa wokovu wangu, Nakungoja Wewe mchana kutwa. |
| 6. | Ee Bwana, kumbuka rehema zako na fadhili zako, Maana zimekuwako tokea zamani. |
| 7. | Usiyakumbuke makosa ya ujana wangu, Wala maasi yangu. Unikumbuke kwa kadiri ya fadhili zako, Ee Bwana kwa ajili ya wema wako. |
| 8. | Bwana yu mwema, mwenye adili, Kwa hiyo atawafundisha wenye dhambi njia. |
| 9. | Wenye upole atawaongoza katika hukumu, Wenye upole atawafundisha njia yake. |
| 10. | Njia zote za Bwana ni fadhili na kweli, Kwao walishikao agano lake na shuhuda zake. |
| 11. | Ee Bwana, kwa ajili ya jina lako, Unisamehe uovu wangu, maana ni mwingi. |
| 12. | Ni nani amchaye Bwana? Atamfundisha katika njia anayoichagua. |
| 13. | Nafsi yake itakaa hali ya kufanikiwa; Wazao wake watairithi nchi. |
| 14. | Siri ya Bwana iko kwao wamchao, Naye atawajulisha agano lake. |
| 15. | Macho yangu humwelekea Bwana daima, Naye atanitoa miguu yangu katika wavu. |
| 16. | Uniangalie na kunifadhili, Maana mimi ni mkiwa na mteswa. |
| 17. | Katika shida za moyo wangu unifanyie nafasi, Na kunitoa katika dhiki zangu. |
| 18. | Utazame teso langu na taabu yangu; Unisamehe dhambi zangu zote. |
| 19. | Uwatazame adui zangu, maana ni wengi, Wananichukia kwa machukio ya ukali. |
| 20. | Unilinde nafsi yangu na kuniponya, Nisiaibike, maana nakukimbilia Wewe. |
| 21. | Ukamilifu na unyofu zinihifadhi, Maana nakungoja Wewe. |
| 22. | Ee Mungu, umkomboe Israeli, Katika taabu zake zote. |
| ← Psalms (25/150) → |