| ← Psalms (21/150) → |
| 1. | Ee Bwana, mfalme atazifurahia nguvu zako, Na wokovu wako ataufanyia shangwe nyingi sana. |
| 2. | Umempa haja ya moyo wake, Wala hukumzuilia matakwa ya midomo yake. |
| 3. | Maana umemsogezea baraka za heri, Umemvika taji ya dhahabu safi kichwani pake. |
| 4. | Alikuomba uhai, ukampa, Muda mrefu wa siku nyingi, milele na milele. |
| 5. | Utukufu wake ni mkuu kwa wokovu wako, Heshima na adhama waweka juu yake. |
| 6. | Maana umemfanya kuwa baraka za milele, Wamfurahisha kwa furaha ya uso wako. |
| 7. | Kwa kuwa mfalme humtumaini Bwana, Na kwa fadhili zake Aliye juu hataondoshwa. |
| 8. | Mkono wako utawapata adui zako wote, Mkono wako wa kuume utawapata wanaokuchukia. |
| 9. | Utawafanya kuwa kama tanuru ya moto, Wakati wa ghadhabu yako. Bwana atawameza kwa ghadhabu yake, Na moto utawala. |
| 10. | Matunda yao utayaharibu na kuyaondoa katika nchi, Na wazao wao katika wanadamu. |
| 11. | Madhali walinuia kukutenda mabaya, Waliwaza hila wasipate kuitimiza. |
| 12. | Kwa maana utawafanya kukupa kisogo, Kwa upote wa uta wako ukiwaelekezea mishale. |
| 13. | Ee Bwana, utukuzwe kwa nguvu zako, Nasi tutaimba na kuuhimidi uweza wako. |
| ← Psalms (21/150) → |