| ← Psalms (148/150) → |
| 1. | Haleluya. Msifuni Bwana kutoka mbinguni; Msifuni katika mahali palipo juu. |
| 2. | Msifuni, enyi malaika wake wote; Msifuni, majeshi yake yote. |
| 3. | Msifuni, jua na mwezi; Msifuni, nyota zote zenye mwanga. |
| 4. | Msifuni, enyi mbingu za mbingu, Nanyi maji mlioko juu ya mbingu. |
| 5. | Na vilisifu jina la Bwana, Kwa maana aliamuru, vikaumbwa. |
| 6. | Amevithibitisha hata milele na milele, Ametoa amri wala haitapita. |
| 7. | Msifuni Bwana kutoka nchi, Enyi nyangumi na vilindi vyote. |
| 8. | Moto na mvua ya mawe, theluji na mvuke, Upepo wa dhoruba ulitendao neno lake. |
| 9. | Milima na vilima vyote, Miti yenye matunda na mierezi yote. |
| 10. | Hayawani, na wanyama wafugwao, Vitambaavyo, na ndege wenye mbawa. |
| 11. | Wafalme wa dunia, na watu wote, Wakuu, na makadhi wote wa dunia. |
| 12. | Vijana waume, na wanawali, Wazee, na watoto; |
| 13. | Na walisifu jina la Bwana, Maana jina lake peke yake limetukuka; Adhama yake i juu ya nchi na mbingu. |
| 14. | Naye amewainulia watu wake pembe, Sifa za watauwa wake wote; Wana wa Israeli, watu walio karibu naye. Haleluya. |
| ← Psalms (148/150) → |