Psalms (147/150)  

1. Haleluya. Msifuni Bwana; Maana ni vema kumwimbia Mungu wetu, Maana kwapendeza, kusifu ni kuzuri.
2. Bwana ndiye aijengaye Yerusalemu, Huwakusanya waliotawanyika wa Israeli.
3. Huwaponya waliopondeka moyo, Na kuziganga jeraha zao.
4. Huihesabu idadi ya nyota, Huzipa zote majina.
5. Bwana wetu ni mkuu na mwingi wa nguvu, Akili zake hazina mpaka.
6. Bwana huwategemeza wenye upole, Huwaangusha chini wenye jeuri.
7. Mwimbieni Bwana kwa kushukuru, Mwimbieni Mungu wetu kwa kinubi.
8. Huzifunika mbingu kwa mawingu, Huitengenezea nchi mvua, Na kuyameesha majani milimani.
9. Humpa mnyama chakula chake, Wana-kunguru waliao.
10. Hapendezwi na nguvu za farasi, Wala hairidhii miguu ya mtu.
11. Bwana huwaridhia wao wamchao, Na kuzitarajia fadhili zake.
12. Msifu Bwana, Ee Yerusalemu; Msifu Mungu wako, Ee Sayuni.
13. Maana ameyakaza mapingo ya malango yako, Amewabariki wanao ndani yako.
14. Ndiye afanyaye amani mipakani mwako, Akushibishaye kwa unono wa ngano.
15. Huipeleka amri yake juu ya nchi, Neno lake lapiga mbio sana.
16. Ndiye atoaye theluji kama sufu, Huimwaga barafu yake kama majivu,
17. Hutupa mvua ya mawe kama makombo, Mbele ya baridi yake ni nani awezaye kusimama?
18. Hulituma neno lake na kuviyeyusha, Huuvumisha upepo wake, maji yakatiririka.
19. Humhubiri Yakobo neno lake, Na Israeli amri zake na hukumu zake.
20. Hakulitendea taifa lo lote mambo kama hayo, Wala hukumu zake hawakuzijua. Haleluya.

  Psalms (147/150)