| ← Psalms (145/150) → |
| 1. | Ee Mungu wangu, Mfalme, nitakutukuza, Nitalihimidi jina lako milele na milele. |
| 2. | Kila siku nitakuhimidi, Nitalisifu jina lako milele na milele. |
| 3. | Bwana ndiye mkuu mwenye kusifiwa sana, Wala ukuu wake hautambulikani. |
| 4. | Kizazi kwa kizazi kitayasifu matendo yako, Kitayatangaza matendo yako makuu. |
| 5. | Nitaifikiri fahari ya utukufu wa adhama yako, Na matendo yako yote ya ajabu. |
| 6. | Watu watayataja matendo yako ya kutisha, Nami nitausimulia ukuu wako. |
| 7. | Watalihubiri kumbukumbu la wema wako mkuu. Wataiimba haki yako. |
| 8. | Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma, Si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, |
| 9. | Bwana ni mwema kwa watu wote, Na rehema zake zi juu ya kazi zake zote. |
| 10. | Ee Bwana, kazi zako zote zitakushukuru, Na wacha Mungu wako watakuhimidi. |
| 11. | Wataunena utukufu wa ufalme wako, Na kuuhadithia uweza wako. |
| 12. | Ili kuwajulisha watu matendo yake makuu, Na utukufu wa fahari ya ufalme wake. |
| 13. | Ufalme wako ni ufalme wa zamani zote, Na mamlaka yako ni ya vizazi vyote. |
| 14. | Bwana huwategemeza wote waangukao, Huwainua wote walioinama chini. |
| 15. | Macho ya watu wote yakuelekea Wewe, Nawe huwapa chakula chao wakati wake. |
| 16. | Waufumbua mkono wako, Wakishibisha kila kilicho hai matakwa yake. |
| 17. | Bwana ni mwenye haki katika njia zake zote, Na mwenye fadhili juu ya kazi zake zote. |
| 18. | Bwana yu karibu na wote wamwitao, Wote wamwitao kwa uaminifu. |
| 19. | Atawafanyia wamchao matakwa yao, Naye atakisikia kilio chao na kuwaokoa. |
| 20. | Bwana huwahifadhi wote wampendao, Na wote wasio haki atawaangamiza. |
| 21. | Kinywa changu kitazinena sifa za Bwana; Wote wenye mwili na walihimidi jina lake takatifu milele na milele. |
| ← Psalms (145/150) → |