← Psalms (144/150) → |
1. | Na ahimidiwe Bwana, mwamba wangu, Anifundishaye mikono yangu vita, Vidole vyangu kupigana. |
2. | Mhisani wangu na boma langu, Ngome yangu na mwokozi wangu, Ngao yangu niliyemkimbilia, Huwatiisha watu wangu chini yangu. |
3. | Ee Bwana, mtu ni kitu gani hata umjue? Na binadamu hata umwangalie? |
4. | Binadamu amefanana na ubatili, Siku zake ni kama kivuli kipitacho. |
5. | Bwana, uziinamishe mbingu zako, ushuke, Uiguse milima nayo itatoka moshi. |
6. | Utupe umeme, uwatawanye, Uipige mishale yako, uwafadhaishe. |
7. | Uinyoshe mikono yako toka juu, uniponye, Unitoe katika maji mengi, katika mkono wa wageni. |
8. | Vinywa vyao vyasema visivyofaa, Na mkono wao wa kuume ni mkono wa uongo. |
9. | Ee Mungu, nitakuimbia wimbo mpya, Kwa kinanda chenye nyuzi kumi nitakuimbia. |
10. | Awapaye wafalme wokovu, Amwokoa Daudi, mtumishi wake, na upanga wa uovu. |
11. | Uniponye, unitoe, Katika mkono wa wageni. Vinywa vyao vyasema visivyofaa, Na mkono wao wa kuume ni mkono wa uongo. |
12. | Wana wetu na wawe kama miche Waliokua ujanani. Binti zetu kama nguzo za pembeni Zilizonakishwa kwa kupamba hekalu. |
13. | Ghala zetu na zijae Zenye akiba za jinsi zote. Kondoo zetu na wazae Elfu na makumi elfu mashambani mwetu. |
14. | Ng'ombe zetu na wachukue mizigo, Kusiwe na kushambuliwa. Wala kusiwe na kuhamishwa, Wala malalamiko katika njia zetu. |
15. | Heri watu wenye hali hiyo, Heri watu wenye Bwana kuwa Mungu wao. |
← Psalms (144/150) → |