| ← Psalms (141/150) → |
| 1. | Ee Bwana, nimekuita, unijie hima, Uisikie sauti yangu nikuitapo. |
| 2. | Sala yangu ipae mbele zako kama uvumba, Kuinuliwa mikono yangu kama dhabihu ya jioni. |
| 3. | Ee Bwana, uweke mlinzi kinywani pangu, Mngojezi mlangoni pa midomo yangu. |
| 4. | Usiuelekeze moyo wangu kunako jambo baya, Nisiyazoelee matendo yasiyofaa, Pamoja na watu watendao maovu; Wala nisile vyakula vyao vya anasa. |
| 5. | Mwenye haki na anipige, itakuwa fadhili; Anikemee, itakuwa kama mafuta kichwani; Kichwa changu kisikatae, Maana siachi kusali kati ya mabaya yao. |
| 6. | Makadhi wao wakiangushwa kando ya genge, Watayasikia maneno yangu, maana ni matamu. |
| 7. | Kama kupasua kuni na kuzichanja juu ya nchi, Ndivyo ilivyo mifupa yetu mdomoni pa kuzimu. |
| 8. | Macho yangu yanakuelekea Wewe, MUNGU Bwana, Nimekukimbilia Wewe, usiniache nafsi yangu. |
| 9. | Unilinde na mtego walionitegea, Na matanzi yao watendao maovu. |
| 10. | Wabaya na waanguke katika nyavu zao wenyewe, Pindi mimi ninapopita salama. |
| ← Psalms (141/150) → |