Psalms (138/150)  

1. Nitakushukuru kwa moyo wangu wote, Mbele ya miungu nitakuimbia zaburi.
2. Nitasujudu nikilikabili hekalu lako takatifu, Nitalishukuru jina lako, Kwa ajili ya fadhili zako na uaminifu wako, Kwa maana umeikuza ahadi yako, Kuliko jina lako lote.
3. Siku ile niliyokuita uliniitikia, Ukanifariji nafsi kwa kunitia nguvu.
4. Ee Bwana, wafalme wote wa dunia watakushukuru, Watakapoyasikia maneno ya kinywa chako.
5. Naam, wataziimba njia za Bwana, Kwa maana utukufu wa Bwana ni mkuu.
6. Ingawa Bwana yuko juu, amwona mnyenyekevu, Naye amjua mwenye kujivuna tokea mbali.
7. Nijapokwenda kati ya shida utanihuisha, Utanyosha mkono juu ya hasira ya adui zangu, Na mkono wako wa kuume utaniokoa.
8. Bwana atanitimilizia mambo yangu; Ee Bwana, fadhili zako ni za milele; Usiziache kazi za mikono yako.

  Psalms (138/150)