← Psalms (135/150) → |
1. | Haleluya. Lisifuni jina la Bwana, Enyi watumishi wa Bwana, sifuni. |
2. | Ninyi msimamao nyumbani mwa Bwana, Nyuani mwa nyumba ya Mungu wenu. |
3. | Msifuni Bwana kwa kuwa Bwana ni mwema, Liimbieni jina lake kwa maana lapendeza. |
4. | Kwa sababu Bwana amejichagulia Yakobo, Na Israeli, wawe watu wake hasa. |
5. | Maana najua mimi ya kuwa Bwana ni mkuu, Na Bwana wetu yu juu ya miungu yote. |
6. | Bwana amefanya kila lililompendeza, Katika mbingu na katika nchi, Katika bahari na katika vilindi vyote. |
7. | Ndiye apandishaye mvuke toka miisho ya nchi; Huifanyia mvua umeme; Hutoa upepo katika hazina zake. |
8. | Aliwapiga wazaliwa wa kwanza wa Misri, Wa wanadamu na wa wanyama. |
9. | Alipeleka ishara na maajabu kati yako, Ee Misri, Juu ya Farao na watumishi wake wote. |
10. | Aliwapiga mataifa mengi, Akawaua wafalme wenye nguvu; |
11. | Sihoni, mfalme wa Waamori, Na Ogu, mfalme wa Bashani, Na falme zote za Kanaani. |
12. | Akaitoa nchi yao iwe urithi, Urithi wa Israeli watu wake. |
13. | Ee Bwana, jina lako ni la milele, Bwana, kumbukumbu lako vizazi hata vizazi. |
14. | Kwa kuwa Bwana atawaamua watu wake, Atawahurumia watumishi wake. |
15. | Sanamu za mataifa ni fedha na dhahabu, Kazi ya mikono ya wanadamu. |
16. | Zina vinywa lakini hazisemi, Zina macho lakini hazioni, |
17. | Zina masikio lakini hazisikii, Wala hamna pumzi vinywani mwake. |
18. | Wazifanyao watafanana nazo, Na kila mmoja anayezitumainia. |
19. | Enyi mlango wa Israeli, mhimidini Bwana; Enyi mlango wa Haruni, mhimidini Bwana; |
20. | Enyi mlango wa Lawi, mhimidini Bwana; Ninyi mnaomcha Bwana, mhimidini Bwana. |
21. | Na ahimidiwe Bwana toka Sayuni, Akaaye Yerusalemu. Haleluya. |
← Psalms (135/150) → |