Psalms (121/150)  

1. Nitayainua macho yangu niitazame milima, Msaada wangu utatoka wapi?
2. Msaada wangu u katika Bwana, Aliyezifanya mbingu na nchi.
3. Asiuache mguu wako usogezwe; Asisinzie akulindaye;
4. Naam, hatasinzia wala hatalala usingizi, Yeye aliye mlinzi wa Israeli.
5. Bwana ndiye mlinzi wako; Bwana ni uvuli mkono wako wa kuume.
6. Jua halitakupiga mchana, Wala mwezi wakati wa usiku.
7. Bwana atakulinda na mabaya yote, Atakulinda nafsi yako.
8. Bwana atakulinda utokapo na uingiapo, Tangu sasa na hata milele.

  Psalms (121/150)