| ← Psalms (119/150) → | 
| 1. | Heri walio kamili njia zao, Waendao katika sheria ya Bwana. | 
| 2. | Heri wazitiio shuhuda zake, Wamtafutao kwa moyo wote. | 
| 3. | Naam, hawakutenda ubatili, Wamekwenda katika njia zake. | 
| 4. | Wewe umetuamuru mausia yako, Ili sisi tuyatii sana. | 
| 5. | Ningependa njia zangu ziwe thabiti, Nizitii amri zako. | 
| 6. | Ndipo mimi sitaaibika, Nikiyaangalia maagizo yako yote. | 
| 7. | Nitakushukuru kwa unyofu wa moyo, Nikiisha kujifunza hukumu za haki yako | 
| 8. | Nitazitii amri zako, Usiniache kabisa | 
| 9. | Jinsi gani kijana aisafishe njia yake? Kwa kutii, akilifuata neno lako. | 
| 10. | Kwa moyo wangu wote nimekutafuta, Usiniache nipotee mbali na maagizo yako. | 
| 11. | Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi. | 
| 12. | Ee Bwana, umehimidiwa, Unifundishe amri zako. | 
| 13. | Kwa midomo yangu nimezisimulia Hukumu zote za kinywa chako. | 
| 14. | Nimeifurahia njia ya shuhuda zako Kana kwamba ni mali mengi. | 
| 15. | Nitayatafakari mausia yako, Nami nitaziangalia njia zako. | 
| 16. | Nitajifurahisha sana kwa amri zako, Sitalisahau neno lako. | 
| 17. | Umtendee mtumishi wako ukarimu, Nipate kuishi, nami nitalitii neno lako. | 
| 18. | Unifumbue macho yangu niyatazame Maajabu yatokayo katika sheria yako. | 
| 19. | Mimi ni mgeni katika nchi, Usinifiche maagizo yako. | 
| 20. | Roho yangu imepondeka kwa kutamani Hukumu zako kila wakati. | 
| 21. | Umewakemea wenye kiburi, Wamelaaniwa waendao mbali na maagizo yako. | 
| 22. | Uniondolee laumu na dharau, Kwa maana nimezishika shuhuda zako. | 
| 23. | Wakuu nao waliketi wakaninena, Lakini mtumishi wako atazitafakari amri zako. | 
| 24. | Shuhuda zako nazo ndizo furaha yangu, Na washauri wangu. | 
| 25. | Nafsi yangu imeambatana na mavumbi, Unihuishe sawasawa na neno lako. | 
| 26. | Nalizisimulia njia zangu ukanijibu, Unifundishe amri zako. | 
| 27. | Unifahamishe njia ya mausia yako, Nami nitayatafakari maajabu yako. | 
| 28. | Nafsi yangu imeyeyuka kwa uzito, Unitie nguvu sawasawa na neno lako. | 
| 29. | Uniondolee njia ya uongo, Unineemeshe kwa sheria yako. | 
| 30. | Nimeichagua njia ya uaminifu, Na kuziweka hukumu zako mbele yangu. | 
| 31. | Nimeambatana na shuhuda zako, Ee Bwana, usiniaibishe. | 
| 32. | Nitakwenda mbio katika njia ya maagizo yako, Utakaponikunjua moyo wangu. | 
| 33. | Ee Bwana, unifundishe njia ya amri zako, Nami nitaishika hata mwisho. | 
| 34. | Unifahamishe nami nitaishika sheria yako, Naam, nitaitii kwa moyo wangu wote. | 
| 35. | Uniendeshe katika mapito ya maagizo yako, Kwa maana nimependezwa nayo. | 
| 36. | Unielekeze moyo wangu na shuhuda zako, Wala usiielekee tamaa. | 
| 37. | Unigeuze macho yangu nisitazame visivyofaa, Unihuishe katika njia yako. | 
| 38. | Umthibitishie mtumishi wako ahadi yako, Inayohusu kicho chako. | 
| 39. | Uniondolee laumu niiogopayo, Maana hukumu zako ni njema. | 
| 40. | Tazama, nimeyatamani mausia yako, Unihuishe kwa haki yako. | 
| 41. | Ee Bwana, fadhili zako zinifikie na mimi, Naam, wokovu wako sawasawa na ahadi yako. | 
| 42. | Nami nitamjibu neno anilaumuye, Kwa maana nalitumainia neno lako. | 
| 43. | Usiliondoe neno la kweli kinywani mwangu kamwe, Maana nimezingojea hukumu zako. | 
| 44. | Nami nitaitii sheria yako daima, Naam, milele na milele. | 
| 45. | Nami nitakwenda panapo nafasi, Kwa kuwa nimejifunza mausia yako. | 
| 46. | Nitazinena shuhuda zako mbele ya wafalme, Wala sitaona aibu. | 
| 47. | Nami nitajifurahisha sana kwa maagizo yako, Ambayo nimeyapenda. | 
| 48. | Na mikono yangu nitayainulia maagizo yako niliyoyapenda, Nami nitazitafakari amri zako. | 
| 49. | Likumbuke neno ulilomwambia mtumishi wako, Kwa sababu umenitumainisha. | 
| 50. | Hii ndiyo faraja yangu katika taabu yangu, Ya kwamba ahadi yako imenihuisha. | 
| 51. | Wenye kiburi wamenidharau mno, Sikujiepusha na sheria zako. | 
| 52. | Nimezikumbuka hukumu zako za kale, Ee Bwana, nikajifariji. | 
| 53. | Ghadhabu imenishika kwa sababu ya wasio haki, Waiachao sheria yako. | 
| 54. | Amri zako zimekuwa nyimbo zangu, Katika nyumba ya ugeni wangu. | 
| 55. | Wakati wa usiku nimelikumbuka jina lako, Ee Bwana, nikaitii sheria yako. | 
| 56. | Hayo ndiyo niliyokuwa nayo, Kwa sababu nimeyashika mausia yako. | 
| 57. | Bwana ndiye aliye fungu langu, Nimesema kwamba nitayatii maneno yake. | 
| 58. | Nimekuomba radhi kwa moyo wangu wote, Unifadhili sawasawa na ahadi yako. | 
| 59. | Nalizitafakari njia zangu, Na miguu yangu nalizielekezea shuhuda zako. | 
| 60. | Nalifanya haraka wala sikukawia, Kuyatii maagizo yako. | 
| 61. | Kamba za wasio haki zimenifunga, Sikuisahau sheria yako. | 
| 62. | Katikati ya usiku nitaamka nikushukuru, Kwa sababu ya hukumu zako za haki. | 
| 63. | Mimi ni mwenzao watu wote wakuchao, Na wale wayatiio mausia yako. | 
| 64. | Bwana, dunia imejaa fadhili zako, Unifundishe amri zako. | 
| 65. | Umemtendea mema mtumishi wako, Ee Bwana, sawasawa na neno lako. | 
| 66. | Unifundishe akili na maarifa, Maana nimeyaamini maagizo yako. | 
| 67. | Kabla sijateswa mimi nalipotea, Lakini sasa nimelitii neno lako. | 
| 68. | Wewe U mwema na mtenda mema, Unifundishe amri zako. | 
| 69. | Wenye kiburi wamenizulia uongo, Kwa moyo wangu wote nitayashika mausia yako. | 
| 70. | Mioyo yao imenenepa kama shahamu, Mimi nimeifurahia sheria yako. | 
| 71. | Ilikuwa vema kwangu kuwa naliteswa, Nipate kujifunza amri zako. | 
| 72. | Sheria ya kinywa chako ni njema kwangu, Kuliko maelfu ya dhahabu na fedha. | 
| 73. | Mikono yako ilinifanya ikanitengeneza, Unifahamishe nikajifunze maagizo yako. | 
| 74. | Wakuchao na wanione na kufurahi, Kwa sababu nimelingojea neno lako. | 
| 75. | Najua ya kuwa hukumu zako ni za haki, Ee Bwana, na kwa uaminifu umenitesa. | 
| 76. | Nakuomba, fadhili zako ziwe faraja kwangu, Sawasawa na ahadi yako kwa mtumishi wako. | 
| 77. | Rehema zako zinijie nipate kuishi, Maana sheria yako ni furaha yangu. | 
| 78. | Wenye kiburi waaibike, maana wamenidhulumu kwa uongo, Mimi nitayatafakari mausia yako. | 
| 79. | Wakuchao na wanirudie, Nao watazijua shuhuda zako. | 
| 80. | Moyo wangu na uwe mkamilifu katika amri zako, Nisije mimi nikaaibika. | 
| 81. | Nafsi yangu imefifia kwa kuutamani wokovu wako, Nimelingojea neno lako. | 
| 82. | Macho yangu yamefifia kwa kuitazamia ahadi yako, Nisemapo, Lini utakaponifariji? | 
| 83. | Maana nimekuwa kama kiriba katika moshi, Sikuzisahau amri zako. | 
| 84. | Siku za mtumishi wako ni ngapi, Lini utakapowahukumu wale wanaonifuatia? | 
| 85. | Wenye kiburi wamenichimbia mashimo, Ambao hawaifuati sheria yako. | 
| 86. | Maagizo yako yote ni amini, Wananifuatia bure, unisaidie. | 
| 87. | Walikuwa karibu na kunikomesha katika nchi, Lakini sikuyaacha mausia yako. | 
| 88. | Unihuishe kwa fadhili zako, Nami nitazishika shuhuda za kinywa chako. | 
| 89. | Ee Bwana, neno lako lasimama Imara mbinguni hata milele. | 
| 90. | Uaminifu wako upo kizazi baada ya kizazi, Umeiweka nchi, nayo inakaa. | 
| 91. | Kwa hukumu zako vimesimama imara hata leo, Maana vitu vyote ni watumishi wako. | 
| 92. | Kama sheria yako isingalikuwa furaha yangu, Hapo ningalipotea katika taabu zangu. | 
| 93. | Hata milele sitayasahau maagizo yako, Maana kwa hayo umenihuisha. | 
| 94. | Mimi ni wako, uniokoe, Kwa maana nimejifunza mausia yako. | 
| 95. | Wasio haki wameniotea ili kunipoteza, Nitazitafakari shuhuda zako. | 
| 96. | Nimeona ukamilifu wote kuwa na mwisho, Bali agizo lako ni pana mno. | 
| 97. | Sheria yako naipenda mno ajabu, Ndiyo kutafakari kwangu mchana kutwa. | 
| 98. | Maagizo yako hunitia hekima kuliko adui zangu, Kwa maana ninayo sikuzote. | 
| 99. | Ninazo akili kuliko wakufunzi wangu wote, Maana shuhuda zako ndizo nizifikirizo. | 
| 100. | Ninao ufahamu kuliko wazee, Kwa kuwa nimeyashika mausia yako. | 
| 101. | Nimeiepusha miguu yangu na kila njia mbaya, Ili nilitii neno lako. | 
| 102. | Sikujiepusha na hukumu zako, Maana Wewe mwenyewe umenifundisha. | 
| 103. | Mausia yako ni matamu sana kwangu, Kupita asali kinywani mwangu. | 
| 104. | Kwa mausia yako najipatia ufahamu, Ndiyo maana naichukia kila njia ya uongo. | 
| 105. | Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu. | 
| 106. | Nimeapa nami nitaifikiliza, Kuzishika hukumu za haki yako. | 
| 107. | Nimeteswa mno; Ee Bwana, unihuishe sawasawa na neno lako. | 
| 108. | Ee Bwana, uziridhie sadaka za kinywa changu, Na kunifundisha hukumu zako. | 
| 109. | Nafsi yangu imo mkononi mwangu daima, Lakini sheria yako sikuisahau. | 
| 110. | Watendao uovu wamenitegea mtego, Lakini sikuikosa njia ya mausia yako. | 
| 111. | Shuhuda zako nimezifanya urithi wa milele, Maana ndizo changamko la moyo wangu. | 
| 112. | Nimeuelekeza moyo wangu nizitende amri zako, Daima, naam, hata milele. | 
| 113. | Watu wa kusita-sita nawachukia, Lakini sheria yako naipenda. | 
| 114. | Ndiwe sitara yangu na ngao yangu, Neno lako nimelingojea. | 
| 115. | Enyi watenda mabaya, ondokeni kwangu, Niyashike maagizo ya Mungu wangu. | 
| 116. | Unitegemeze sawasawa na ahadi yako, nikaishi, Wala usiniache niyaaibikie matumaini yangu. | 
| 117. | Unisaidie nami nitakuwa salama, Nami nitaziangalia amri zako daima. | 
| 118. | Umewakataa wote wazikosao amri zako, Kwa maana hila zao ni uongo. | 
| 119. | Wabaya wa nchi pia umewaondoa kama takataka, Ndiyo maana nimezipenda shuhuda zako. | 
| 120. | Mwili wangu unatetemeka kwa kukucha Wewe, Nami ninaziogopa hukumu zako. | 
| 121. | Nimefanya hukumu na haki, Usiniache mikononi mwao wanaonionea. | 
| 122. | Uwe mdhamini wa mtumishi wako, apate mema, Wenye kiburi wasinionee. | 
| 123. | Macho yangu yamefifia kwa kuutamani wokovu wako, Na ahadi ya haki yako. | 
| 124. | Kama zilivyo rehema zako umtendee mtumishi wako, Na amri zako unifundishe. | 
| 125. | Mimi ni mtumishi wako, unifahamishe, Nipate kuzijua shuhuda zako. | 
| 126. | Wakati umewadia Bwana atende kazi; Kwa kuwa wameitangua sheria yako. | 
| 127. | Ndiyo maana nimeyapenda maagizo yako, Kuliko dhahabu, naam, dhahabu iliyo safi. | 
| 128. | Maana nayaona mausia yako yote kuwa ya adili, Kila njia ya uongo naichukia. | 
| 129. | Shuhuda zako ni za ajabu, Ndiyo maana roho yangu imezishika. | 
| 130. | Kufafanusha maneno yako kwatia nuru, Na kumfahamisha mjinga. | 
| 131. | Nalifunua kinywa changu nikatweta, Maana naliyatamani maagizo yako. | 
| 132. | Unigeukie, unirehemu mimi, Kama iwahusuvyo walipendao jina lako. | 
| 133. | Uzielekeze hatua zangu kwa neno lako, Uovu usije ukanimiliki. | 
| 134. | Unikomboe na dhuluma ya mwanadamu, Nipate kuyashika mausia yako. | 
| 135. | Umwangazie mtumishi wako uso wako, Na kunifundisha amri zako. | 
| 136. | Macho yangu yachuruzika mito ya maji, Kwa sababu hawaitii sheria yako. | 
| 137. | Ee Bwana, Wewe ndiwe mwenye haki, Na hukumu zako ni za adili. | 
| 138. | Umeziagiza shuhuda zako kwa haki, Na kwa uaminifu mwingi. | 
| 139. | Juhudi yangu imeniangamiza, Maana watesi wangu wameyasahau maneno yako. | 
| 140. | Neno lako limesafika sana, Kwa hiyo mtumishi wako amelipenda. | 
| 141. | Mimi ni mdogo, nadharauliwa, Lakini siyasahau mausia yako. | 
| 142. | Haki yako ni haki ya milele, Na sheria yako ni kweli. | 
| 143. | Taabu na dhiki zimenipata, Maagizo yako ni furaha yangu. | 
| 144. | Haki ya shuhuda zako ni ya milele, Unifahamishe, nami nitaishi. | 
| 145. | Nimeita kwa moyo wangu wote; Ee Bwana, uitike; Nitazishika amri zako. | 
| 146. | Nimekuita Wewe, uniokoe, Nami nitazishika shuhuda zako. | 
| 147. | Kutangulia mapambazuko naliomba msaada, Naliyangojea maneno yako kwa tumaini. | 
| 148. | Macho yangu yalitangulia makesha ya usiku, Ili kuitafakari ahadi yako. | 
| 149. | Uisikie sauti yangu sawasawa na fadhili zako, Ee Bwana, unihuishe sawasawa na hukumu yako. | 
| 150. | Wanakaribia wanaonifuatia kwa chuki, Wamekwenda mbali na sheria yako. | 
| 151. | Ee Bwana, Wewe U karibu, Na maagizo yako yote ni kweli. | 
| 152. | Tokea zamani nimejua kwa shuhuda zako, Ya kuwa umeziweka zikae milele. | 
| 153. | Uyaangalie mateso yangu, uniokoe, Maana sikuisahau sheria yako. | 
| 154. | Unitetee na kunikomboa, Unihuishe sawasawa na ahadi yako. | 
| 155. | Wokovu u mbali na wasio haki, Kwa maana hawajifunzi amri zako. | 
| 156. | Ee Bwana, rehema zako ni nyingi, Unihuishe sawasawa na hukumu zako. | 
| 157. | Wanaonifuatia na watesi wangu ni wengi, Lakini sikujiepusha na shuhuda zako. | 
| 158. | Nimewaona watendao uhaini nikachukizwa, Kwa sababu hawakulitii neno lako. | 
| 159. | Uangalie niyapendavyo mausia yako, Ee Bwana, unihuishe sawasawa na fadhili zako. | 
| 160. | Jumla ya neno lako ni kweli, Na kila hukumu ya haki yako ni ya milele. | 
| 161. | Wakuu wameniudhi bure, Ila moyo wangu unayahofia maneno yako. | 
| 162. | Naifurahia ahadi yako, Kama apataye mateka mengi. | 
| 163. | Nimeuchukia uongo, umenikirihi, Sheria yako nimeipenda. | 
| 164. | Mara saba kila siku nakusifu, Kwa sababu ya hukumu za haki yako. | 
| 165. | Wana amani nyingi waipendao sheria yako, Wala hawana la kuwakwaza. | 
| 166. | Ee Bwana, nimeungojea wokovu wako, Na maagizo yako nimeyatenda. | 
| 167. | Nafsi yangu imezishika shuhuda zako, Nami nazipenda mno. | 
| 168. | Nimeyashika mausia yako na shuhuda zako, Maana njia zangu zote zi mbele zako. | 
| 169. | Ee Bwana, kilio changu na kikukaribie, Unifahamishe sawasawa na neno lako. | 
| 170. | Dua yangu na ifike mbele zako, Uniponye sawasawa na ahadi yako. | 
| 171. | Midomo yangu na itoe sifa, Kwa kuwa unanifundisha mausia yako. | 
| 172. | Ulimi wangu na uiimbe ahadi yako, Maana maagizo yako yote ni ya haki. | 
| 173. | Mkono wako na uwe tayari kunisaidia, Maana nimeyachagua mausia yako. | 
| 174. | Ee Bwana, nimeutamani wokovu wako, Na sheria yako ndiyo furaha yangu. | 
| 175. | Nafsi yangu na iishi, ipate kukusifu, Na hukumu zako zinisaidie. | 
| 176. | Nimetanga-tanga kama kondoo aliyepotea; Umtafute mtumishi wako; Kwa maana sikuyasahau maagizo yako. | 
| ← Psalms (119/150) → |