← Psalms (115/150) → |
1. | Ee Bwana, kutukuza usitutukuze sisi, Bali ulitukuze jina lako, Kwa ajili ya fadhili zako, Kwa ajili ya uaminifu wako. |
2. | Kwa nini mataifa kusema, Yuko wapi Mungu wao? |
3. | Lakini Mungu wetu yuko mbinguni, Alitakalo lote amelitenda. |
4. | Sanamu zao ni fedha na dhahabu, Kazi ya mikono ya wanadamu. |
5. | Zina vinywa lakini hazisemi, Zina macho lakini hazioni, |
6. | Zina masikio lakini hazisikii, Zina pua lakini hazisikii harufu, |
7. | Mikono lakini hazishiki, miguu lakini haziendi, Wala hazitoi sauti kwa koo zake. |
8. | Wazifanyao watafanana nazo, Kila mmoja anayezitumainia. |
9. | Enyi Israeli, mtumainini Bwana; Yeye ni msaada wao na ngao yao. |
10. | Enyi mlango wa Haruni, mtumainini Bwana; Yeye ni msaada wao na ngao yao. |
11. | Enyi mmchao Bwana, mtumainini Bwana; Yeye ni msaada wao na ngao yao. |
12. | Bwana ametukumbuka, Naye atatubariki sisi. Ataubariki mlango wa Israeli, Ataubariki mlango wa Haruni, |
13. | Atawabariki wamchao Bwana, Wadogo kwa wakubwa. |
14. | Bwana na awaongeze ninyi, Ninyi na watoto wenu. |
15. | Na mbarikiwe ninyi na Bwana, Aliyezifanya mbingu na nchi. |
16. | Mbingu ni mbingu za Bwana, Bali nchi amewapa wanadamu. |
17. | Sio wafu wamsifuo Bwana, Wala wo wote washukao kwenye kimya; |
18. | Bali sisi tutamhimidi Bwana, Tangu leo na hata milele. |
← Psalms (115/150) → |