| ← Psalms (109/150) → |
| 1. | Ee Mungu wa sifa zangu, usinyamaze, |
| 2. | Kwa maana wamenifumbulia kinywa; Kinywa cha mtu asiye haki, cha hila, Wamesema nami kwa ulimi wa uongo. |
| 3. | Naam, kwa maneno ya chuki wamenizunguka, Wamepigana nami bure. |
| 4. | Badala ya upendo wangu wao hunishitaki, Ijapokuwa naliwaombea. |
| 5. | Wamenichukuza mabaya badala ya mema, Na chuki badala ya upendo wangu. |
| 6. | Uweke mtu mkorofi juu yake, Mshitaki asimame mkono wake wa kuume. |
| 7. | Katika kuhukumiwa ataonekana hana haki, Na sala yake itadhaniwa kuwa ni dhambi. |
| 8. | Siku zake na ziwe chache, Usimamizi wake na atwae mtu mwingine. |
| 9. | Wanawe na wawe yatima, Na mkewe na awe mjane. |
| 10. | Kutanga na watange wanawe na kuomba, Watafute chakula mbali na mahame yao. |
| 11. | Mdai na anase vitu vyote alivyo navyo, Wageni na wateke mapato ya kazi yake. |
| 12. | Asiwe na mtu wa kumfanyia fadhili, Wala mtu wa kuwahurumia yatima wake. |
| 13. | Wazao wake waangamizwe, Jina lao likafutwe katika kizazi cha pili. |
| 14. | Uovu wa baba zake ukumbukwe mbele za Bwana, Na dhambi ya mamaye isifutwe. |
| 15. | Ziwe mbele za Bwana daima, Aliondoe kumbukumbu lao duniani. |
| 16. | Kwa kuwa hakukumbuka kutenda fadhili, Bali alimfukuza mnyonge na mhitaji, Hata akamfisha mtu aliyevunjika moyo, |
| 17. | Naye alipenda kulaani, nako kukampata. Hakupendezwa na kubariki, kukawa mbali naye, |
| 18. | Alijivika laana kana kwamba ni vazi lake. Ikamwingilia moyoni kama maji, Na kama mafuta mifupani mwake. |
| 19. | Na iwe kwake kama vazi ajivikalo, Na kama mshipi ajifungao daima. |
| 20. | Ndiyo malipo ya washitaki wangu toka kwa Bwana, Na ya hao wanaoisingizia nafsi yangu mabaya. |
| 21. | Na Wewe, MUNGU, Bwana, unitendee kwa ajili ya jina lako, Kwa kuwa fadhili zako ni njema uniokoe. |
| 22. | Kwa maana mimi ni mnyonge na mhitaji, Na moyo wangu umejeruhi ndani yangu. |
| 23. | Ninapita kama kivuli kianzacho kutoweka, Ninapeperushwa kama nzige. |
| 24. | Magoti yangu yamedhoofu kwa kufunga, Na mwili wangu umekonda kwa kukosa mafuta. |
| 25. | Nami nalikuwa laumu kwao, Wanionapo hutikisa vichwa vyao. |
| 26. | Ee Bwana, Mungu wangu, unisaidie, Uniokoe sawasawa na fadhili zako. |
| 27. | Nao wakajue ya kuwa ndio mkono wako; Wewe, Bwana, umeyafanya hayo. |
| 28. | Wao walaani, bali Wewe utabariki, Wameondoka wao wakaaibishwa, Bali mtumishi wako atafurahi. |
| 29. | Washitaki wangu watavikwa fedheha, Watajivika aibu yao kama joho. |
| 30. | Nitamshukuru Bwana kwa kinywa changu, Naam, nitamsifu katikati ya mkutano. |
| 31. | Maana atasimama mkono wa kuume wa mhitaji Amwokoe na wanaoihukumu nafsi yake. |
| ← Psalms (109/150) → |