| ← Psalms (107/150) → |
| 1. | Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, Kwa maana fadhili zake ni za milele. |
| 2. | Na waseme hivi waliokombolewa na Bwana, Wale aliowakomboa na mkono wa mtesi. |
| 3. | Akawakusanya kutoka nchi zote, Mashariki na magharibi, kaskazini na kusini. |
| 4. | Walitanga-tanga jangwani katika njia ya nyika; Hawakuona mji wa kukaa. |
| 5. | Waliona njaa, waliona na kiu, Nafsi yao ilikuwa ikizimia ndani yao. |
| 6. | Wakamlilia Bwana katika dhiki zao, Akawaponya na shida zao. |
| 7. | Akawaongoza kwa njia ya kunyoka, Wapate kwenda mpaka mji wa kukaa. |
| 8. | Na wamshukuru Bwana, kwa fadhili zake, Na maajabu yake kwa wanadamu. |
| 9. | Maana hushibisha nafsi yenye shauku, Na nafsi yenye njaa huijaza mema. |
| 10. | Waliokaa katika giza na uvuli wa mauti, Wamefungwa katika taabu na chuma, |
| 11. | Kwa sababu waliyaasi maneno ya Mungu, Wakalidharau shauri lake Aliye juu. |
| 12. | Hata akawadhili moyo kwa taabu, Wakajikwaa wala hakuna msaidizi. |
| 13. | Wakamlilia Bwana katika dhiki zao, Akawaponya na shida zao. |
| 14. | Aliwatoa katika giza na uvuli wa mauti, Akayavunja mafungo yao. |
| 15. | Na wamshukuru Bwana kwa fadhili zake, Na maajabu yake kwa wanadamu. |
| 16. | Maana ameivunja milango ya shaba, Ameyakata mapingo ya chuma. |
| 17. | Wapumbavu, kwa sababu ya ukosaji wao, Na kwa sababu ya maovu yao, hujitesa. |
| 18. | Nafsi zao zachukia kila namna ya chakula, Wameyakaribia malango ya mauti. |
| 19. | Wakamlilia Bwana katika dhiki zao, Akawaponya na shida zao. |
| 20. | Hulituma neno lake, huwaponya, Huwatoa katika maangamizo yao. |
| 21. | Na wamshukuru Bwana kwa fadhili zake, Na maajabu yake kwa wanadamu. |
| 22. | Na wamtolee dhabihu za kushukuru, Na kuyasimulia matendo yake kwa kuimba. |
| 23. | Washukao baharini katika merikebu, Wafanyao kazi yao katika maji mengi, |
| 24. | Hao huziona kazi za Bwana, Na maajabu yake vilindini. |
| 25. | Maana husema, akavumisha upepo wa dhoruba, Ukayainua juu mawimbi yake. |
| 26. | Wapanda mbinguni, watelemka vilindini, Nafsi yao yayeyuka kwa hali mbaya. |
| 27. | Wayumba-yumba, wapepesuka kama mlevi, Akili zao zote zawapotea. |
| 28. | Wakamlilia Bwana katika dhiki zao, Akawaponya na shida zao. |
| 29. | Huituliza dhoruba, ikawa shwari, Mawimbi yake yakanyamaza. |
| 30. | Ndipo walipofurahi kwa kuwa yametulia Naye huwaleta mpaka bandari waliyoitamani. |
| 31. | Na wamshukuru Bwana kwa fadhili zake, Na maajabu yake kwa wanadamu. |
| 32. | Na wamtukuze katika kusanyiko la watu, Na wamhimidi katika baraza ya wazee. |
| 33. | Amegeuza mito ikawa jangwa, Na chemchemi za maji zikawa nchi ya kiu. |
| 34. | Nchi ya matunda mengi ikawa uwanda wa chumvi, Kwa sababu ya ubaya wao walioikaa. |
| 35. | Amegeuza jangwa ikawa ziwa la maji, Na nchi kavu ikawa chemchemi za maji. |
| 36. | Maana amewakalisha huko wenye njaa, Nao wametengeneza mji wa kukaa. |
| 37. | Wakapanda mbegu katika mashamba, Na kutia mizabibu iliyotoa matunda yake. |
| 38. | Naye huwabariki wakaongezeka sana, Wala hayapunguzi makundi yao. |
| 39. | Kisha wakapungua na kudhilika, Kwa kuonewa na mabaya na huzuni. |
| 40. | Akawamwagia wakuu dharau, Na kuwazungusha katika nyika isiyo na njia. |
| 41. | Akamweka mhitaji juu mbali na mateso, Akamfanyia jamaa kama kundi la kondoo. |
| 42. | Wanyofu wa moyo wataona na kufurahi, Na uovu wa kila namna utajifumba kinywa. |
| 43. | Aliye na hekima na ayaangalie hayo; Na wazitafakari fadhili za Bwana. |
| ← Psalms (107/150) → |