Psalms (103/150)  

1. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana. Naam, vyote vilivyo ndani yangu Vilihimidi jina lake takatifu.
2. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana, Wala usizisahau fadhili zake zote.
3. Akusamehe maovu yako yote, Akuponya magonjwa yako yote,
4. Aukomboa uhai wako na kaburi, Akutia taji ya fadhili na rehema,
5. Aushibisha mema uzee wako, Ujana wako ukarejezwa kama tai;
6. Bwana ndiye afanyaye mambo ya haki, Na hukumu kwa wote wanaoonewa.
7. Alimjulisha Musa njia zake, Wana wa Israeli matendo yake.
8. Bwana amejaa huruma na neema, Haoni hasira upesi, ni mwingi wa fadhili.
9. Yeye hatateta sikuzote, Wala hatashika hasira yake milele.
10. Hakututenda sawasawa na hatia zetu, Wala hakutulipa kwa kadiri ya maovu yetu.
11. Maana mbingu zilivyoinuka juu ya nchi, Kadiri ile ile rehema zake ni kuu kwa wamchao.
12. Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi, Ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi.
13. Kama vile baba awahurumiavyo watoto wake, Ndivyo Bwana anavyowahurumia wamchao.
14. Kwa maana Yeye anatujua umbo letu, Na kukumbuka ya kuwa sisi tu mavumbi.
15. Mwanadamu siku zake zi kama majani; Kama ua la kondeni ndivyo asitawivyo.
16. Maana upepo hupita juu yake, kumbe haliko! Na mahali pake hapatalijua tena.
17. Bali fadhili za Bwana zina wamchao Tangu milele hata milele, Na haki yake ina wana wa wana;
18. Maana, wale walishikao agano lake, Na kuyakumbuka maagizo yake ili wayafanye.
19. Bwana ameweka kiti chake cha enzi mbinguni, Na ufalme wake unavitawala vitu vyote.
20. Mhimidini Bwana, enyi malaika zake, Ninyi mlio hodari, mtendao neno lake, Mkiisikiliza sauti ya neno lake.
21. Mhimidini Bwana, enyi majeshi yake yote, Ninyi watumishi wake mfanyao mapenzi yake.
22. Mhimidini Bwana, enyi matendo yake yote, Mahali pote pa milki yake. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.

  Psalms (103/150)