| ← Psalms (10/150) → |
| 1. | Ee Bwana, kwa nini wasimama mbali? Kwani kujificha nyakati za shida? |
| 2. | Kwa kiburi chake asiye haki mnyonge anafuatiwa kwa ukali; Na wanaswe kwa hila zizo hizo walizoziwaza. |
| 3. | Maana mdhalimu hujisifia tamaa ya nafsi yake, Na mwenye choyo humkana Bwana na kumdharau. |
| 4. | Mdhalimu kwa kiburi cha uso wake Asema, Hatapatiliza. Jumla ya mawazo yake ni, Hakuna Mungu; |
| 5. | Njia zake ni thabiti kila wakati. Hukumu zako ziko juu asizione, Adui zake wote awafyonya. |
| 6. | Asema moyoni mwake, Sitaondoshwa, Kizazi baada ya kizazi sitakuwamo taabuni. |
| 7. | Kinywa chake kimejaa laana, Na hila na dhuluma. Chini ya ulimi wake kuna madhara na uovu, |
| 8. | Hukaa katika maoteo ya vijiji. Mahali pa siri humwua asiye na hatia, Macho yake humvizia mtu duni. |
| 9. | Huotea faraghani kama simba pangoni, Huotea amkamate mtu mnyonge. Naam, humkamata mtu mnyonge, Akimkokota wavuni mwake. |
| 10. | Hujikunyata na kuinama; Watu duni huanguka kwa nguvu zake. |
| 11. | Asema moyoni mwake, Mungu amesahau, Auficha uso wake, haoni kamwe. |
| 12. | Bwana, uondoke, Ee Mungu, uuinue mkono wako, Usiwasahau wanyonge. |
| 13. | Kwani mdhalimu kumdharau Mungu. Akisema moyoni mwake, Hutapatiliza? |
| 14. | Umeona, maana unaangalia madhara na jeuri, Uyatwae mkononi mwako. Mtu duni hukuachia nafsi yake, Maana umekuwa msaidizi wa yatima. |
| 15. | Uuvunje mkono wake mdhalimu, Na mbaya, uipatilize dhuluma yake, hata usiione. |
| 16. | Bwana ndiye Mfalme milele na milele; Mataifa wamepotea kutoka nchi yake. |
| 17. | Bwana, umeisikia tamaa ya wanyonge, Utaitengeneza mioyo yao, utalitega sikio lako. |
| 18. | Ili kumhukumu yatima naye aliyeonewa, Binadamu aliye udongo asizidi kudhulumu. |
| ← Psalms (10/150) → |