← Proverbs (9/31) → |
1. | Hekima umeijenga nyumba yake, Amezichonga nguzo zake saba; |
2. | Amechinja nyama zake, umechanganya divai yake, Ameiandalia meza yake pia. |
3. | Amewatuma wajakazi wake, analia, Mahali pa mjini palipoinuka sana, |
4. | Kila aliye mjinga na aingie humu. Tena amwambia mtu aliyepungukiwa na akili, |
5. | Njoo ule mkate wangu, Ukanywe divai niliyoichanganya. |
6. | Enyi wajinga, acheni ujinga, mkaishi, Mkaende katika njia ya ufahamu. |
7. | Amkemeaye mwenye dharau hujipatia fedheha; Amkaripiaye mtu mbaya hujipatia aibu. |
8. | Usimkaripie mwenye dharau, asije akakuchukia; Mkaripie mwenye hekima, naye atakupenda. |
9. | Mwelimishe mwenye hekima, naye atazidi kuwa na hekima; Mfundishe mwenye haki, naye atazidi kuwa na elimu; |
10. | Kumcha Bwana ni mwanzo wa hekima; Na kumjua Mtakatifu ni ufahamu. |
11. | Maana, kwa msaada wangu siku zako zitazidishwa; Na miaka ya maisha yako itaongezwa. |
12. | Kama una hekima, una hekima kwa nafsi yako; Na kama una dharau, utaichukua peke yako. |
13. | Mwanamke mpumbavu hupiga kelele, Ni mjinga, hajui kitu. |
14. | Hukaa mlangoni pa nyumba yake, Juu ya kiti mahali pa mjini palipoinuka, |
15. | Apate kuwaita wapitao njiani, Waendao moja kwa moja katika njia zao. |
16. | Kila aliye mjinga na aingie humu. Tena amwambia mtu aliyepungukiwa na akili, |
17. | Maji yaliyoibiwa ni matamu, Na mkate ulioliwa kwa siri hupendeza. |
18. | Lakini huyo hajui ya kuwa wafu wamo humo; Ya kuwa wageni wake wamo chini kuzimuni. |
← Proverbs (9/31) → |