Proverbs (8/31)  

1. Je! Hekima halii? Ufahamu hatoi sauti yake?
2. Juu ya mahali palipoinuka karibu na njia, Penye njia panda, ndipo asimamapo.
3. Karibu na malango, mahali pa kuingia mjini, Mahali pa kuyaingilia malango anapiga kelele.
4. Enyi watu, nawaita ninyi; Na sauti yangu ni kwa wanadamu.
5. Enyi wajinga, fahamuni werevu, Nanyi wapumbavu, mpate moyo wa kufahamu.
6. Sikieni, maana nitasema yaliyo mazuri, Na kufumbua midomo yangu kutakuwa maadili.
7. Maana kinywa changu kitasema kweli, Na uovu ni chukizo kwa midomo yangu.
8. Maneno yote ya kinywa changu yana haki; Hapana hata neno lililopotoka au la ukaidi.
9. Yote humwelea yule afahamuye, Yote huelekea mbele yao waliopata maarifa.
10. Pokea mafundisho yangu, wala si fedha, Na maarifa kuliko dhahabu safi.
11. Maana hekima ni bora kuliko marijani; Wala vyote vinavyotamanika havilingani nayo.
12. Mimi, hekima, nimefanya werevu kuwa kao langu; Natafuta maarifa na busara.
13. Kumcha Bwana ni kuchukia uovu; Kiburi na majivuno, na njia mbovu, Na kinywa cha ukaidi pia nakichukia.
14. Shauri ni langu, na maarifa yaliyo sahihi; Mimi ni ufahamu, mimi nina nguvu.
15. Kwa msaada wangu wafalme humiliki, Na wakuu wanahukumu haki.
16. Kwa msaada wangu wakuu hutawala, Na waungwana, naam, waamuzi wote wa dunia.
17. Nawapenda wale wanipendao, Na wale wanitafutao kwa bidii wataniona.
18. Utajiri na heshima ziko kwangu, Naam, utajiri udumuo, na haki pia.
19. Matunda yangu hupita dhahabu, naam, dhahabu safi, Na faida yangu hupita fedha iliyo teule.
20. Natembea katika njia ya haki, Katikati ya mapito ya hukumu.
21. Niwarithishe mali wale wanipendao, Tena nipate kuzijaza hazina zao.
22. Bwana alikuwa nami katika mwanzo wa njia yake, Kabla ya matendo yake ya kale.
23. Nalitukuka tokea milele, tangu awali, Kabla haijawako dunia.
24. Wakati visipokuwako vilindi nalizaliwa, Wakati zisipokuwako chemchemi zilizojaa maji.
25. Kabla milima haijawekwa imara, Kabla ya vilima nalizaliwa.
26. Alipokuwa hajaiumba dunia, wala makonde Wala chanzo cha mavumbi ya dunia;
27. Alipozithibitisha mbingu nalikuwako; Alipopiga duara katika uso wa bahari;
28. Alipofanya imara mawingu yaliyo juu; Chemchemi za bahari zilipopata nguvu;
29. Alipoipa bahari mpaka wake, Kwamba maji yake yasiasi amri yake; Alipoiagiza misingi ya nchi;
30. Ndipo nilipokuwa pamoja naye, kama stadi wa kazi; Nikawa furaha yake kila siku; Nikifurahi daima mbele zake;
31. Nikiifurahia dunia inayokaliwa na watu; Na furaha yangu ilikuwa pamoja na wanadamu.
32. Basi, wanangu, nisikilizeni sasa; Maana heri hao wazishikao amri zangu.
33. Sikieni mafundisho, mpate hekima, Wala msiikatae.
34. Ana heri mtu yule anisikilizaye, Akisubiri sikuzote malangoni pangu, Akingoja penye vizingiti vya milango yangu.
35. Maana yeye anionaye mimi aona uzima, Naye atapata kibali kwa Bwana.
36. Bali anikosaye hujidhuru nafsi yake mwenyewe, Na wao wanichukiao hupenda mauti.

  Proverbs (8/31)